Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, imeadhimisha Mwezi wa Maendeleo ya Jamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho hayo, yamefanyika Septemba 30, 2026, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, ambapo washiriki walipatiwa elimu kupitia mada mbalimbali zinazohusu maendeleo ya jamii.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni lishe, ukatili wa kijinsia, malezi na ulinzi wa watoto, fursa za kiuchumi, pamoja na utaratibu wa upatikanaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa asilimia 10 kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, amesema Idara ya Maendeleo ya Jamii ina jukumu kubwa zaidi ya utoaji wa mikopo, kwani inahusika pia na kuhamasisha maendeleo na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili jamii katika nyanja za kiuchumi, kielimu na kijamii.
Bi. Quintine amesema Serikali inatambua umuhimu wa wataalamu wa maendeleo ya jamii katika kuleta mabadiliko chanya, ndiyo maana imeendelea kuajiri watumishi wenye taaluma hiyo ili kusaidia jamii kukabiliana na changamoto na kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo.
Aidha, amewataka wataalamu wa maendeleo ya jamii kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa wananchi, hususan kuhusu athari za ajira za watoto, pamoja na kuhamasisha wazazi kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu bila kubaguliwa kwa misingi ya jinsia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bw. Hosea Mwabusila, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa nasaha na maelekezo aliyoyatoa, akiahidi kuwa idara hiyo itayafanyia kazi ili kuendelea kukuza ustawi wa wananchi na kujenga jamii bora.
Katika hafla hiyo pia alikuwepo Afisa Utumishi wa Wilaya ya Urambo, Bw. Matheo Mathew, pamoja na viongozi na makundi mbalimbali ya wananchi.
Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Familia Imara, Jamii Imara na Taifa Imara kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.”
Discussion
Reader comments
0 contributions