Skip to main content

URAIBU USIOONEKANA: SIMU ZINAWAJENGA VIJANA AU ZINAWAMEZA KIMYA KIMYA?

Na Gideon Gregory - Dodoma.

URAIBU USIOONEKANA: SIMU ZINAWAJENGA VIJANA AU ZINAWAMEZA KIMYA KIMYA? 

Na Gideon Gregory - Dodoma.

Kuamka na simu mkononi, kuitazama kila baada ya dakika chache na kulala ukiwa bado upo mtandaoni ni jambo lililozoeleka kwa vijana wengi.

Lakini je, ni matumizi ya kawaida ya teknolojia au ni ishara ya uraibu usioonekana unaokua kimya kimya?

Utangulizi.

Vijana wengi kila wanapoamka asubuhi, jambo la kwanza wanalolifanya ni kuchukua, ambapo dakika chache za kupitia jumbe na mitandao ya kijamii hugeuka kuwa saa nzima na wengine wanapoingia kazini, ujikuta wakifungua simu kila baada ya dakika chache, na usiku hulala baada ya kutumia saa kadhaa mtandaoni.

Mitazamo.

Edward ni kijana anayeishi Dodoma, yeye anakiri kuwa kila anapoamka asubuhi huikimbilia simu yake na kuanza kupitia jumbe mbalimbali hasa katika mitandao ya kijamii ili kuweza kuweka akili yake sawa. 

Kwa upande wake Rebeka ana mtazamo tofauti juu ya matumizi hayo ya simu na mitandao ya kijamii, ambapo anadai kuwa mara nyingi suala hilo huweza kuathiri maisha kwani kuna muda utamani kufanya jambo fulani lakini mwisho wa siku ujikuta akiangukia kwenye kushika simu na kuanza kufuatilia yanayojiri mitandaoni. 

Kwa wengi, matumizi ya simu na mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha ya kila siku. Lakini wataalamu wanaonya kuwa matumizi yanapokosa mipaka yanaweza kugeuka kuwa kile wanachokiita uraibu usioonekana.

Dalili.

Florah Wadutya ni Mwanasaikolojia na Mshauri Nasaha, anasema dalili za uraibu huu ni pamoja na kukosa utulivu mtu anapokuwa mbali na simu yake.

"Ili tuweze kujua na kugundua kuwa kijana huyu ana dalili zinazoonesha matumizi ya simu au mitandao yamegeuka kuwa uraibu, hata akisikia tu mlio wa sauti ya simu unaoendana na wakwake anahisi ni ya kwake tayari ameshatoa mfukoni simu yake anashika na kuanza kuangalia kumbe pengine mlio wa simu ya mtu mwingine," alisema. 

Anaongeza kuwa hata anapokuwa amelala kwenye masikio yake anasikia kama kuna simu inaita au inatetema, jambo ambalo linadhihilisha uraibu wa matumizi ya simu. 

Kwanini Vijana?

Mchambuzi wa masuala ya vijana na mwanasheria Zainabu Hassan anaeleza kuwa kizazi cha sasa kimekulia katika mazingira ambayo teknolojia ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, hivyo vijana ukutana na shinikizo la kutaka kuendana na kasi ya taarifa na kujilinganisha na wengine kupitia mitandao ya kijamii.

Anasema vijana hukutana na shinikizo la kutaka kuendana na kasi ya taarifa, kujilinganisha na wengine kupitia mitandao ya kijamii na kutafuta uthibitisho kupitia likes, maoni na idadi ya wafuasi.

"Leo vijana wengi wamezaliwa kwenye ulimwengu wa kidigitali lakini hatujawaandaa vya kutosha kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia, mitandao ya kijamii hugeuka sehemu ya maisha yao lakini imejenga utamaduni wa kutafuta umaarufu wa haraka kuliko mafanikio ya kweli," anasema.

Vijana wengi wanapima thamani yao kwa kuwa na wafuasi wengi na likes baadala ya kutumia maarifa, ujuzi, ubunifu na kutangaza kazi zao ambapo hali hiyo inaitaja kuzalisha kizazi kinachotumia muda mwingi sana kujionesha kuliko kujijenga hatua ambayo inaathiri maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Athari zinazoonekana polepole.

Mbali na kupunguza umakini katika masomo na kazi, wataalamu wanasema matumizi kupita kiasi ya simu yanaweza kuathiri muda wa kupumzika, mawasiliano ya ana kwa ana na uwezo wa mtu kujikita katika shughuli muhimu.

Kwa baadhi ya vijana, muda unaotumika mtandaoni huanza kuchukua nafasi ya muda wa familia, marafiki na shughuli nyingine za maendeleo binafsi.

Suluhisho.

Wataalamu hao wanashauri vijana kuweka muda maalumu wa matumizi ya simu na kujenga utamaduni wa kufanya shughuli zisizohusisha skrini kama vile michezo, kusoma vitabu na kushiriki shughuli za kijamii.

Aidha, wazazi, walimu na jamii wanahimizwa kuzungumza kwa uwazi na vijana kuhusu matumizi salama ya teknolojia badala ya kutumia marufuku pekee.

Takwimu za hivi karibuni, zinaonesha kuwa idadi ya watu duniani imefikia zaidi ya bilioni 8.2 huku watumiaji wa simu za mkononi wakiwa zaidi ya bilioni 5.78, na wale wanaotumia mitandao ya kijamii wakiwa zaidi ys bilioni 5.24.

Ambapo vijana hutumia wastani wa saa 2 hadi 4 kwa siku kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya burudani, mawasiliano, na biashara.

Kwasasa teknolojia imebadilisha namna dunia inavyojifunza, kufanya kazi na kuwasiliana. Lakini kadiri inavyoendelea kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, ndivyo umuhimu wa kuitumia kwa uwiano unavyoongezeka.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.