Jumla ya nyumba 42 zimeezuliwa kufuatia mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali katika Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, huku vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Nyarutuntu vikiharibika pamoja na baadhi ya migomba kuanguka.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitun Msofe, amesema nyumba 17 zimeezuliwa katika kijiji cha Nyarutuntu na nyingine 25 katika kijiji cha Chanyangabwa, huku kaya 42 zikiathirika.

Msofe amesema hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa wala kupoteza maisha kutokana na tukio hilo, huku idadi kamili ya wananchi walioathirika ikiwa bado haijabainishwa.

Amesema kwa sasa, baadhi ya wakazi ambao nyumba zao zimeharibika wamepata hifadhi kwa ndugu na jamaa zao huku wakiendelea na maandalizi ya kurekebisha makazi yao.

Aidha, amewataka wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua, kufuatia utabiri wa uwezekano wa kunyesha kwa mvua zinazozidi wastani, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Discussion
Reader comments
0 contributions