Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Matendo ya huruma ni moja kati ya silaha kubwa ambayo inanogesha ukaribu kati ya jamii na taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi, matendo ambayo yanabeba tafsiri ya utu na mioyo ya dhahabu kwa wale wanaotoa kwa ajili ya wasiojiweza.
Kwa mara ya kwanza mkoani Simiyu, Umoja wa Polisi Wanaume unaundwa na kuigusa jamii moja kwa moja kwa kuchangia vifaa vya shule kwa wototo zaidi ya 600 wenye uhitaji, katika Shule ya Msingi Sima A na Sima B zilizopo mjini Bariadi, ambao inaaridiwa kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kuwapatia mahitaji hayo yakiwa ni pamoja na viatu vya shule, mashati, sketi, soksi na kaptula.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Muasisi wa Umoja huo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi a Polisi Mkoani Simiyu, Sunday Songwe amesema kuwa kilichowagusa kuanzisha umoja huo ni baada ya kushuhudia wanawake kuwa mstari wa mbele katika kufanya matendo ya huruma kwa watoto na wenye uhitaji ilhali wanaume wapo na hakuna wanachofanya.

Amesema, “sisi wanaume tunavaa suti tunapita mitaani wengine kutwa wapo kwenye sehemu za starehe na kwingineko na baadhi yetu tumetelekeza familia tunasahau kama wapo watoto wengi wenye uhitaji ambao tunaweza tukawastiri kwa kupunguza kitu kimoja katika starehe tunazofanya,wanawake ndio huwa stari wa mbele kufanya matendo haya ,nikajiuliza nini kinashindikana kwa wanaume?.”
Songwe ameongeza kuwa, ”siku ya maadhimisho ya Wanawake Duniani tuliambatana kuja hapa na Polisi wanawake kuleta chochote kitu katika shule hii,lakini hali ambayo tuliwakuta nayo hawa watoto ni huzuni kubwa,"

"Baada ya hapo nikaona si sawa kwa nini nisiwalete pamoja polisi Wanaume tuone namna ya kuwastiri watoto ambao wanatembea bila viatu,wanavaa kandambili,kaptula zimechanika makalioni na kulibeba vifuani mwetu kama wazazi ndipo tukaafikiana kuwavisha."
Hata hivyo, amesisitiza Umoja huo hautoishia katika kusaidia wanafunzi bali watazunguka katika maeneo mbalimbali mkoani humo kuangalia watu wenye uhitaji zaidi katika vituo vya watoto yatima,familia duni na hata shule ili kuona ni namna gani wanaweza kuwazaidia ili nao wajisijione tofauti na wenzao wenye uwezo huku baadae wakiona namna ya kuwajumuisha na wanaume wengine wa taasisi zingine wanaowiwa kutoa misaada kwa jamii zao.

Kwa upande wa Uongozi wa shule hizo, wao wamekiri kitendo hicho kuwa ni cha kuonesha utu, kwani watoto watafikisha ujumbe kwa wazazi na kuongeza kujiamini darasani na hatimaye ufaulu kuongezeka.
“Kuna kipindi mtoto anashindwa hata kuleta kazi kwa mwalimu akijiona jinsi alivyo ,anakosa kujiamini kuwa jambo fulani anaweza watoto wengine hujisaidia darasani anashindwa tu kutembea mbele ya darasa na wenzake kwa sababu nguo zake zimechanika anaamua kukaa hapo mapumziko wakitoka naye ndio atoke,” alisema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sima A, Dalbert Chambia.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Sima B, Mawazo Masanja amesema, “hii itaongeza hata ufaulu mtoto anaweza kutembea mbele ya wenzake bila woga na kushiriki michezo kwa sababu hawa wasio na mahitaji yote huwa wanajinyanyapaa wenyewe na kunyanyapaliwa na wenzao ,kwa kweli wanapitia mengi lakini kitendo hiki niwape kongole jeshi la Polisi."

Akiongea kwa niaba ya wanafunzi waliopokea misaada hiyo, mwanafunzi wa darasa la nne, Angel Daniel ametoa shukrani kwa Jeshi la Polisi kwa kuwaona na kuahidi kuongeza bidii katika masomo kwani wazazi wake hawakuwa na chochote cha kuwasaidia.
“Mimi sikuwa na viatu wala shati nilipewa viatu kwa msaada na mtu huko mtaani ila vilikuwa vikubwa sana nikivaa shuleni wenzangu wananiita mimi kubwa jinga kwa sababu viatu vilinizidi,wananisimanga najisikia vibaya lakini leo ndiyo nimeona nguvu ya jeshi la polisi siamini kama wamenivalisha, baba sijui yuko wapi hata tukimpigia hapatikani,mama hana hela ya kuninunulia nguo nawaahidi nitasoma sana ili nifaulu asante jeshi la polisi,” alisema Angel.
Discussion
Reader comments
0 contributions