Na Daniel Gahu - Katavi.
Serikali ya Mkoa wa Katavi kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa, Albert Msovela amesema, Mkoa wa Katavi umejipanga kwenda kushindana kikamilifu katika mashindano ya UMISSETA ngazi ya kitaifa badala ya kushiriki pekee, akieleza kuwa maandalizi yaliyofanyika yanaupa mkoa matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga rasmi kambi ya michezo ya wanafunzi iliyodumu kwa siku nne, ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya UMISSETA ngazi ya Taifa, ambapo amewapongeza walimu, makocha na wanafunzi kwa kujitoa kwao katika kujiandaa na mashindano hayo.

Amebainisha kiwango cha maandalizi pamoja na nidhamu iliyooneshwa kambini vinaashiria kuwa Mkoa wa Katavi unaenda kuonesha ushindani mkubwa na kuipeperusha vyema bendera ya mkoa huo katika mashindano ya UMISSETA kitaifa.
Aidha, amewataka viongozi watakaoambatana na wanamichezo hao kuhakikisha wanawatunza na kuwalinda wakati wote wa safari na mashindano ili warejee salama kama walivyoondoka.

“Nina imani Mkoa wa Katavi utaenda kufanya vizuri. Hatuendi kushiriki pekee, tunaenda kushindana,” amesema Bw. Msovela huku akiwatakia safari njema wanamichezo hao.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Katavi, George Mtawa, amesema michezo ni sanaa, ajira na njia muhimu ya kuibua na kukuza vipaji kwa vijana.

Amesema mashindano hayo ya UMISSETA yamewezesha vipaji mbalimbali kuonekana, huku akisisitiza huo si mwisho bali ni mwanzo wa safari ya maendeleo ya vipaji hivyo.
Jumla ya wanafunzi 600 wameshiriki katika kambi hiyo iliyohusisha michezo 10 tofauti kwa muda wa siku nne, ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya UMISSETA ngazi ya taifa yatakayofanyika mkoani Iringa.






Discussion
Reader comments
0 contributions