Skip to main content

UMEME WAKWAMISHA SHUGHULI BANDARI YA KAREMA, RC MRINDOKO ATOA AGIZO KWA TANESCO

Kukatikakatika kwa huduma ya umeme mara kwa mara katika Bandari ya Karema mkoani Katavi kumeanza kuathiri shughuli za uendeshaji wa bandari hiyo, hali iliyomlazimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, kutoa agizo la hatua za haraka kuchukuliwa.

UMEME WAKWAMISHA SHUGHULI BANDARI YA KAREMA, RC MRINDOKO ATOA AGIZO KWA TANESCO
Studio Narration JAMBO FM

UMEME WAKWAMISHA SHUGHULI BANDARI YA KAREMA, RC MRINDOKO ATO...

0:00 --:--

Kukatikakatika kwa huduma ya umeme mara kwa mara katika Bandari ya Karema mkoani Katavi kumeanza kuathiri shughuli za uendeshaji wa bandari hiyo, hali iliyomlazimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, kutoa agizo la hatua za haraka kuchukuliwa.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika bandari hiyo, Mrindoko amemuagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Katavi kufika katika eneo hilo haraka na kushughulikia changamoto hiyo, akisisitiza kuwa hataki kuona huduma ya umeme ikiendelea kuwa kikwazo katika shughuli za bandari yenye umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Mkoa wa Katavi.

“Ninahitaji kesho Meneja wa TANESCO Mkoa afike hapa atatue kero hii. Kama haiko ndani ya uwezo wao, ninawaagiza kuanzia Mkurugenzi wao huko juu waje watatue kero ya umeme katika bandari hii ambayo ina manufaa makubwa sana katika Mkoa wetu wa Katavi,” amesema Mrindoko.

Agizo hilo limekuja baada ya taarifa ya uendeshaji wa Bandari ya Karema kubainisha kuwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kumekuwa kukikwamisha baadhi ya shughuli za bandari, hali inayoweza kuathiri ufanisi wa huduma, usafirishaji wa bidhaa na shughuli za wafanyabiashara wanaotegemea bandari hiyo.

Changamoto hiyo imepewa uzito zaidi kutokana na umuhimu wa Bandari ya Karema katika kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji, ikiwemo biashara zinazohusisha maeneo ya ndani ya Tanzania pamoja na nchi jirani.

Pamoja na kutoa agizo hilo, Mkuu wa Mkoa ameupongeza uongozi na watendaji wa Bandari ya Karema kwa kazi wanayoifanya, akisema maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shughuli za biashara na usafirishaji.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya usimamizi wa shughuli katika bandari hapa. Hii inatokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali ambayo yameongeza uwezo wa Bandari ya Karema na kufungua fursa kubwa zaidi za biashara ndani ya nchi na nchi jirani,” amesema Mrindoko.

Mrindoko amesema kuimarika kwa bandari hiyo kuna nafasi kubwa katika kuchochea biashara na uchumi wa Mkoa wa Katavi, huku akiwataka watendaji kuendelea kutoa huduma kwa weledi na ufanisi, pamoja na kuhakikisha miundombinu iliyowekezwa inatumika kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na wafanyabiashara.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa TANESCO kuona kama agizo hilo litazaa majibu ya haraka, huku wadau wa Bandari ya Karema wakisubiri kurejea kwa huduma ya umeme yenye uhakika ili shughuli za biashara na usafirishaji ziendelee bila vikwazo vinavyotokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.