Skip to main content

UKATILI WA KIJINSIA: HDI YAWAJENGEA UWEZO WASICHANA WAELIMISHA RIKA GEITA

Na Ibrahim Rojala - Geita.

UKATILI WA KIJINSIA: HDI YAWAJENGEA UWEZO WASICHANA WAELIMISHA RIKA GEITA

Na Ibrahim Rojala - Geita.

Shirika lisilo la Kiserikali la Human Dignity Initiative (HDI) limeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wasichana waelimisha rika kutoka katika kata za Nyankumbu, Mtakuja, Nyawilimilwa, Nkome na Lwamgasa iliyofanyika katika Manispaa ya Geita Mkoani Geita ambao wanatarajiwa kwenda kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia ndani ya kata hizo.

Elimu hiyo imetolewa kwa lengo la kuwapa ujuzi wa uwasilishaji wa elimu ya upatikanaji wa haki kwa manusura wa matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  Mradi wa Justice for Survivors, unaolenga kuwawezesha kiuchumi, kijamii pamoja na kuwasaidia kupata haki baada ya kupitia ukatili wa kijinsia,unaotekelezwa na  Shirika lisilo la Kiserikali la Human Dignity Initiative (HDI) ndani ya kata hizo.

Baada ya kukamilika kwa  mafunzo hayo baadhi ya wasichana  ambao ni manusura wa ukatili wa mimba za utotoni kutoka ndani ya kata hizo tano wamesema umaskini ndani ya  jamii Mkoani Geita umekuwa kikwazo kikubwa cha makabiliano ya ukatili wa kijinsia hususani katika maeneo yenye shughuli nyingi za kiuchumi ndani ya kata zao.

“Kuna mabinti wenye umri mdogo au rika balehe wanaopata ujauzito katika umri mdogo kutokana na umasikini wa familia lakini pia changamoto nyingine inayojitokeza katika mazingira ya migodini ni changamoto za ajira za utotoni na migogoro ya kifamilia,”

“Mama na baba wanapotengana wanaacha watoto ambao wanakimbilia kufanya kazi ndogo ndogo migodini,” ameeleza Tausi Juma kutoka kata ya Lwamgasa  ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa mafunzo yaliyotolewa.

Kwa upande wake kinara wa ukatili wa kijinsia, Grace Emmanuel kutoka kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita ameeleza kuwa mwingiliano mkubwa wa kibiashara uliopo katika kata hiyo umekuwa ukitumiwa kama fursa kwa baadhi ya wazazi kuwatumia watoto wadogo kufanya biashara ndogo ndogo ambazo wakati mwingine zimekuwa zikiwaweka katika hatari ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Nashukuru kwa haya mafunzo tuliyopewa na shirika la HDI, haya mafunzo yananisaidia juu ya namna gani ninakwenda kuwasaidia watoto kupata haki zao za msingi na ili wasifanyiwe ukatili wa kijinsia maana wanahitaji kusoma na wana ndoto za kesho yao zilizo kubwa,kupitia mafunzo haya tumeona madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia chanzo kikubwa kikiwa ni umaskini,” ameeleza Grace.

Mwakilishi wa Human Dignity Initiative (HDI), Wakili Walta Carlos amesema ili kukabiliana na changamoto ya umasikini,kupitia mradi huo watawajengea uwezo na kuwawezesha kiuchumi pamoja na kutambua na kubadili changamoto zilizo ndani ya jamii zao kuwa fursa za kiuchumi.

“Tunategemea kupitia mashujaa hawa ambao wamepatiwa mafunzo watakwenda kuifikia jamii na hasa vikundi vya mabinti ambao walipata ujauzito wakiwa katika umri mdogo,na tunaona kwamba  mabinti wengi hasa ambao wanapata ujauzito katika umri mdogo na ambao wanapitia ukatili mbalimbali wamekuwa wakiwa nyuma katika suala zima la kuinuka kiuchumi,kupitia program hii pia tutakwenda kujengea uwezo mabinti hawa,” amebainisha Wakili Walta.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Afisa Maendeleo ya Jamii  kutoka kata ya Nkome halmashauri ya wilaya ya Geita Benjamin Alexander Morris amelishukuru Shirika la HDI kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika makabiliano ya ukatili wa kijinsia na kueleza kwamba wanakwenda kushirikiana na shirika hilo kupinga ukatili kwa kutumia nyenzo mbalimbali kama vile kuvifikia vituo vyenye mikusanyiko mingi ya vijana kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili.

Hatua hii ni ya mwanzo katika kuwafikia zaidi ya wasichana 250 kutoka kata hizo tano  Mkoani Geita waliokatisha masomo kutokana na ujauzito wanatarajiwa kunufaika na Mradi wa Justice for Survivors, unaolenga kuwawezesha kiuchumi na kijamii pamoja na kuwasaidia kupata haki baada ya kupitia ukatili wa kijinsia.

Mradi huo unatekelezwa  kwa kipindi cha mwaka mmoja ndani ya kata tano zilizochaguliwa na ukitarajiwa kuongeza uelewa wa kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia,kuibua vinara wa kupinga ukatili wa kijinsia,kuongeza ubunifu na uelewa wa masuala ya ujasiriamali kwa wasichana lengwa.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.