Skip to main content

UKAGUZI HESABU ZA MWAKA : HALMASHAURIBUKOBA KUPATA HATI SAFI

Na Clavery Christian, Bukoba – Kagera.

UKAGUZI HESABU ZA MWAKA : HALMASHAURIBUKOBA KUPATA HATI SAFI

Na Clavery Christian, Bukoba – Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 5.1, sawa na asilimia 114.57 ya makadirio hadi Mei 2026.

Kanali Kido alitoa pongezi hizo Juni 18, 2026, wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mafanikio hayo yanaonyesha usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na kujituma kwa viongozi pamoja na watendaji wa halmashauri katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

Pamoja na pongezi hizo, Kanali Kido alitoa maelekezo mbalimbali ya kuimarisha utendaji wa halmashauri, ikiwemo kuendelea kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa kifedha wa halmashauri.

Aidha, alisisitiza matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Malipo ya Serikali (GePG) katika huduma zote za afya, akibainisha kuwa mfumo huo umeongeza uwazi, uwajibikaji na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.

Kanali Kido pia alielekeza halmashauri kuendelea kutenga na kupeleka fedha za mapato ya ndani kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, ikiwemo kutenga asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na asilimia 10 kwa Mfuko wa Mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Theophil Elieza, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitikia mwaliko wa kushiriki kikao hicho muhimu na kuahidi kuwa madiwani kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri watahakikisha maagizo yote yaliyotolewa yanatekelezwa ipasavyo.

Alisema halmashauri itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato, uwajibikaji wa fedha za umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Bukoba.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.