Na Daniel Gahu - Katavi.
Ujenzi wa Daraja la Mafunsi lenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3 unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Mpanda, huku Serikali ikilenga kuondoa changamoto ya usafiri inayowakabili wananchi, hususan wakati wa msimu wa mvua.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, linalounganisha Kata ya Itenka katika Halmashauri ya Nsimbo na Kata ya Mwamkulu katika Manispaa ya Mpanda.
Mhe. Jamila amesema kukamilika kwa daraja hilo kutafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo, kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuwezesha wananchi kufikia masoko na huduma mbalimbali kwa urahisi.

“Kukamilika kwa daraja hili kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo haya,” amesema Jamila.
Amesema maeneo yanayounganishwa na daraja hilo yana mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi, hivyo uwepo wa miundombinu bora ya usafiri utasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.
Kwa mujibu wa Mhe. Jamila, changamoto ya kuvuka eneo hilo imekuwa kubwa zaidi wakati wa msimu wa mvua, hali ambayo imekuwa ikiathiri usafiri wa wananchi pamoja na usafirishaji wa bidhaa.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kwa wakati kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, kwa kuwa utawawezesha kutumia njia hiyo kwa usalama na urahisi bila vikwazo vinavyosababishwa na mvua.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema utekelezaji wa mradi huo unaakisi dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuboresha miundombinu na huduma za msingi ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jamila amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi bila kuathiri ubora, akisisitiza kuwa daraja hilo linapaswa kukamilika kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo kwa wakati kutawawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao bila kukumbana na changamoto za usafiri zinazojitokeza mara kwa mara wakati wa mvua.
Vilevile, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka daraja hilo kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo mara baada ya kukamilika, ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.
Daraja la Mafunsi linatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu ya miundombinu inayotarajiwa kuimarisha muunganiko wa maeneo ya Wilaya ya Mpanda na kuchochea zaidi biashara, usafirishaji na shughuli nyingine za kiuchumi kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions