Na Ibrahim Rojala - Geita.
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa na stendi ya kisasa katika Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu ya biashara na usafiri.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya miradi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Harun Fashe, wakati wa ziara ya Waziri wa Madini na Mlezi na mwangalizi wa shughuli za Maendeleo wa Mkoa wa Geita,Waziri wa Madini , Antony Mavunde, alisema hadi sasa miradi hiyo imegharimu jiasi cha shilingi bilioni 4 na utekelezaji umefikia asilimia 46.

Alisema mkataba wa ujenzi ulisainiwa Machi 24, 2025 kati ya Halmashauri na Mkandarasi China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Ltd, huku mradi ukitarajiwa kukamilika ifikapo 28 Desemba 2027.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe,Paskas Muragili alimhakikishia Waziri Mavunde kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Naye Waziri wa madini,Antony Mavunde, alipongeza uongozi wa Mkoa wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na kuwataka kuendelea kuhakikisha inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa ili kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi ya kimkakati.


Discussion
Reader comments
0 contributions