Na Saulo Stephen - Singida.
Ujenzi wa Soko la Kimataifa la Vitunguu unaoendelea katika eneo la Kititimo, Manispaa ya Singida, umefikia asilimia 41, huku ukitarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 3.9 utakapokamilika.
Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuimarisha biashara ya zao la vitunguu na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida.

Soko hilo linajengwa chini ya Mradi wa TACTIC unaotekelezwa katika Manispaa ya Singida kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 24.7. Kupitia mradi huo, Serikali inalenga kuboresha miundombinu ya biashara na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi pamoja na kuongeza mapato kwa wananchi.
Mbali na ujenzi wa soko hilo, Mradi wa TACTIC pia unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita saba pamoja na mtaro wa kilomita mbili. Miundombinu hiyo inatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza gharama za usafiri na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Kukamilika kwa soko hilo kunatarajiwa kuifanya Singida kuwa kitovu kikuu cha biashara ya vitunguu nchini na kuongeza ushindani wa zao hilo katika masoko ya ndani na nje ya nchi, hatua itakayowanufaisha wakulima na wadau wote wa mnyororo wa thamani wa zao la vitunguu.
Discussion
Reader comments
0 contributions