Skip to main content

UJENZI JENGO LA UTAWALA HALMASHAURI YA MULEBA WAIVA

Na Clavery Christian, Muleba - Kagera.

UJENZI JENGO LA UTAWALA HALMASHAURI YA MULEBA WAIVA

Na Clavery Christian, Muleba - Kagera.

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Aprili 2, 2026 imesaini mkataba wa ujenzi wa jengo jipya la utawala lenye thamani ya shilingi bilioni sita, fedha zilizotolewa na Serikali kuu, ambapo mradi huo utakelezwa na kampuni ya SUMA JKT Construction Company Ltd.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Magongo Justus, alimtaka mkandarasi kuandaa mpango kazi madhubuti na unaotekelezeka ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa.

Magongo alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu wa mradi huo kwa kuhakikisha kuwa kila hatua ya ujenzi inazingatia ubora unaotakiwa, sambamba na kutumia rasilimali kwa ufanisi ili kuleta thamani halisi ya fedha za Serikali katika mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Isaya Mbenje, alisema kuwa jengo hilo la ghorofa moja litakuwa na ofisi za idara zote pamoja na vitengo, hatua itakayorahisisha uratibu wa shughuli za kiutendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mbenje alipongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na usimamizi madhubuti wa rasilimali na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata huduma bora zaidi kupitia miundombinu hiyo mipya.

Naye Meneja wa Kanda ya Ziwa Magharibi wa SUMA JKT Construction Company Ltd, Meja Hamadi Matata ameihakikishia halmashauri ya wilaya ya Muleba kuwa watatekeleza mradi huo kwa ubora wa hali ya juu na kuhakikisha unakamilika ndani ya muda wa mwaka mmoja kama ilivyokubaliwa katika mkataba.

Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, Evart Kagaruki amesema, ujenzi wa jengo hilo utaongeza ari ya watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya kiutawala katika ngazi za halmashauri.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.