Skip to main content

UHARIBIFU WA TEMBO: TANAPA IJENGE KITUO CHA ASKARI WA UHIFADHI KARAGWE - DKT. KIJAJI

Na Cecilia Shiratu, Karagwe - Kagera.

UHARIBIFU WA TEMBO: TANAPA IJENGE KITUO CHA ASKARI WA UHIFADHI   KARAGWE - DKT. KIJAJI

Na Cecilia Shiratu, Karagwe - Kagera.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Askari wa Uhifadhi wilayani Karagwe, ili kudhibiti uvamizi wa Tembo unaosababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Dkt. Kijaji ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea ombi la Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, aliyeeleza changamoto ya uvamizi wa tembo unaoathiri wananchi wa kata za Rugu, Rugera, Kihanga, Nyakabanga na Nyakakika.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakabanga, Waziri huyo amesema Serikali imejipanga kutafuta suluhisho la kudumu kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi ili kumaliza kero ya uvamizi wa wanyamapori.

Aidha, ameeleza kuwa wananchi ambao mazao yao yameharibiwa na tembo katika maeneo hayo watalipwa fedha za kifuta jasho zenye jumla ya shilingi milioni 39 ndani ya siku saba.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Nyakakika na kusema Serikali tayari imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. 

Amesema fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 250 zitatolewa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ili kukamilisha mradi huo na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha wakulima wa Wilaya ya Karagwe na Mkoa wa Kagera kunufaika na bei nzuri ya zao la kahawa, hali iliyochochea ongezeko la kipato kwa wakulima.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.