Na Ibrahim Rojala - Geita.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia na linaendelea kumchunguza Amina Shabani (21), mkazi wa Kijiji na Kata ya Muungano, Wilaya ya Chato, kwa tuhuma za kumfukia mtoto wake mchanga wa jinsia ya kike akiwa hai ndani ya shimo muda mfupi baada ya kujifungua.
Tukio hilo linadaiwa kutendeka Mei 16, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri nyumbani kwake, masaa machache baada ya kujifungua siku hiyo majira ya saa 4:00 asubuhi kabla ya kubainika Mei 17, 2026 majira ya saa 1:00 usiku baada ya wananchi kusikia sauti ya mtoto mchanga kutoka nyuma ya nyumba ya mtuhumiwa bila kuonekana mtoto yeyote.
Jeshi la Polisi lilifika na kumuokoa mtoto huyo, kuanza uchunguzi na kumfikisha Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu na uchunguzi wa kitabibu, ambapo alifariki dunia Mei 18, 2026 majira ya saa 10:00 alasiri.

Aidha, baada ya kutenda tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na kujificha kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria. Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kubaini alipokimbilia na kujificha na kumkamata akiwa katika harakati za kutoroka kwenda mkoa jirani. Chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa, na uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuimarisha malezi na uangalizi kwa wanawake wajawazito na waliojifungua kujifungua ili kuhakikisha wanapata msaada wa haraka wa kijamii, kisaikolojia na kiafya unaoweza kuzuia matukio ya aina hii na kuokoa maisha ya watoto wachanga.
Discussion
Reader comments
0 contributions