Na Daniel Gahu - Katavi.
Wakati Serikali ikiendelea kuboresha mazingira rafiki ya ufanyaji wa kazi kwa watumishi wa Umma, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewataka viongozi wa Halmashauri na taasisi za umma mkoani Katavi kuiga utamaduni wa kuwajali watumishi kwa kuboresha mazingira yao ya kazi, akisema hatua hiyo ni msingi wa kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari jipya la usafiri wa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, RC Mrindoko amesema chombo hicho kinapaswa kuwa motisha kwa watumishi kuongeza uwajibikaji na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Amesema Serikali ya Mkoa inatarajia kuona mabadiliko chanya katika utoaji huduma hospitalini hapo, ikiwemo kupungua kwa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi kuhusu huduma za afya katika hospitali hiyo.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali kuiga mfano huo kwa kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wao, hususan wale wanaofanya kazi katika maeneo ya mbali, ili kuongeza morali ya kazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Deogratius Banuba, amesema uongozi wa hospitali hiyo uliona umuhimu wa kupunguza gharama za usafiri kwa watumishi wake, jambo lililopelekea kutenga fedha kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ununuzi wa gari hilo kupitia mapato ya ndani ya hospitali.
Ameongeza na kusema gari hilo lenye thamani ya shilingi milioni 178 linatarajiwa kurahisisha usafiri wa watumishi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Kwa upande wao watumishi wa hospitali hiyo wamesema usafiri huo ni motisha kwao kwani utafanya waongeze bidii zaidi katika kutoa huduma bora kwa wateja pindi watakapo fika hospitalini hapo kupata huduma za kitabibu.





Discussion
Reader comments
0 contributions