Serikali imesema iko tayari kuchukua hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunga migodi, endapo itabainika kuwa wamiliki na waendeshaji wake wanakiuka kanuni za usalama na kuhatarisha maisha ya wachimbaji.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, wakati akizungumza na wachimbaji, wamiliki mameneja wa migodi na maafisa madini katika Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga, katika mafunzo yanayolenga kuongeza uelewa kuhusu usalama wa migodi wakati wa kipindi cha mvua kubwa kinachotarajiwa.

Amesema maisha ya mchimbaji yana thamani kubwa kwa familia, jamii na Taifa, hivyo masuala ya uzalishaji hayapaswi kutangulizwa mbele ya usalama wa binadamu.
“Tutakuwa wakali na tutachukua hatua kwa mujibu wa Sheria na kanuni zilizopo, hasa zile za usimamizi wa mazingira na usalama migodini, na ikiwezekana tutafunga migodi,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo siyo chaguo linalopendelewa kwa sababu shughuli za madini zina mchango mkubwa katika uchumi na ajira, lakini Serikali haiwezi kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea endapo maisha ya wachimbaji yanawekwa hatarini.
Akizungumzia kipindi cha mvua kubwa za El-Nino zinazotarajiwa Samamba amesema migodi inapaswa kuweka taratibu maalum za kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kusimamisha shughuli za chini ya ardhi wakati mvua kubwa ikiendelea na kuruhusu wachimbaji kuingia baada ya eneo kukaguliwa na kuthibitishwa kuwa salama.

Aidha, ametoa maagizo ya kuongezwa kwa ukaguzi wa mabwawa ya mabaki ya migodi (TSF) akitaka kuhakikisha mabwawa hayo yana uwezo na uimara wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua kubwa, huku kingo zake na maeneo mengine muhimu yakikaguliwa mara kwa mara.
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa, amewataka wachimbaji wa madini Wilayani humo kuzingatia usalama katika shughuli zao, hususan katika msimu huu unaotarajiwa kuwa na kiwango kikubwa cha mvua, akisema maji yanaweza kusababisha madhara katika maeneo yao.
Ameiomba Wizara ya Madini kuendelea na mpango wa kuwawezesha wachimbaji kupata vifaa vya uchimbaji, ikiwemo Compressor, winchi, vifaa vya kupondea,kuchoronga pamoja na mashine za kusaga mawe, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uzalishaji.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu tawala Wilaya ya Kahama, Tumshukuru Mdui amesema Wilaya ya Kahama imejiandaa katika kukabiliana na dharura zitakazojitokeza wakati wa mvua za El-Nino huku akiwataka wachimbaji kuchukua tahadhari mapema kulingana na hali ya hewa na kuendelea kufuatilia matangazo ya Serikali ili kupata taarifa sahihi za hali ya hewa.

Discussion
Reader comments
0 contributions