Na Tryphone Odace - Kigoma.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma kimesema kinaendelea kuisimamia Serikali kuhakikisha Ilani ya Chama inatekelezwa kikamilifu, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuchochea maendeleo ya wananchi.
Miongoni mwa miradi inayosisitizwa ni Mradi wa Umwagiliaji wa Mto Luiche pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ambayo chama hicho kinaeleza kuwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza leo, Agosti 10, 2026, baada ya kikao cha Halmashauri Kuu iliyoboreshwa ya CCM Mkoa wa Kigoma, kilichowajumuisha viongozi wa Jumuiya za Chama ngazi ya Kata, Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Christopher Pallangyo, amesema chama hicho kitaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Pallangyo amesema kikao hicho kililenga kujadili na kutathmini masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya chama, pamoja na kuwakumbusha na kuwahimiza wanachama kutimiza wajibu wao, ikiwemo kulipa ada za uanachama kwa wakati.
Amesema ili CCM iendelee kuaminiwa na wananchi na kubaki kuwa chama kinachoongoza, ni muhimu kuhakikisha miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi inatekelezwa kwa wakati.
“Ili chama kiendelee kuwepo madarakani na kuaminiwa na wananchi, ni lazima miradi ya maendeleo inayogusa wananchi itekelezwe kwa wakati,” amesema Pallangyo.

Akizungumzia namna CCM inavyoendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi, Pallangyo amesema chama hicho kinaendelea kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Kigoma.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Serikali inakwenda sambamba na matarajio ya wananchi na yale yaliyoainishwa katika Ilani ya CCM.
Aidha, amewahimiza wanachama kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na kuchangia maendeleo yake ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wao, baadhi ya wanachama walioshiriki katika kikao hicho wamesema CCM inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali inayotokana na chama hicho.
Wamesema usimamizi huo ni muhimu katika kuhakikisha yale yaliyoahidiwa na kuandikwa katika Ilani ya CCM yanatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.
Wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kuongeza imani ya wananchi kwa chama na Serikali yake.
Discussion
Reader comments
0 contributions