Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi Wilbroad Mutafungwa, amewataka wakazi wa wilaya ya Ukerewe kuacha kuendeleza imani potofu zinazoweza kusababisha taharuki katika jamii.
Akizungumza na wananchi, Kamanda Mtafungwa alisisitiza kuwa baadhi ya taarifa zinazosambazwa zinachochewa na watu wachache wenye nia ya kujipatia maslahi binafsi, jambo linaloweza kuvuruga amani na utulivu wa eneo hilo.
Onyo hilo linakuja kufuatia kusambaa kwa taarifa zinazodai kuwa mkazi mmoja wa Ukerewe alimezwa na mamba na baadaye kurejea akiwa hai baada ya siku saba.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa madai hayo hayana uthibitisho wa kisayansi wala ushahidi wa kuaminika.
“Ni muhimu kwa wananchi kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho na badala yake kuzingatia taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka husika,” alisema Kamanda Mtafungwa.
Aidha, amewahimiza wakazi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi ili kudhibiti upotoshaji.
Discussion
Reader comments
0 contributions