Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Chama kikuu cha ushirika Kahama (KACU) Kwa kushirikiana na bodi ya tumbaku Tanzania mkoa wa kitumbaku Kahama wamefanya ziara katika vyama vya msingi vya ushirika kwa lengo la kutoa semina kwa wakulima kuhusu jinsi ya kufunga tumbaku bora na kuacha kuchanganya madaraja ya tumbaku na uchafu.
Akizungumza katika semina hiyo mwenyekiti wa chama kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) Emmanuel Nyambi amewata wakulima kuacha kuchanganya Ngulai kwenye Tumbaku zao kwani kufanya hivyo kutasababisha wanunuzi wa Tumbaku kukimbia Kwenda kununua Tumbaku kwingine.

“Tujitahidi sana turudishe Imani kwa wanunuzi wetu,tunapoweka uchafu kwenye tumbaku na mawe ndiyo yanayoleta ugumu wa bei na kupata bei ya chini kutokana na hii ya kuchafua tumbaku ili tupate kilo nyingi” Amesema Nyambi.
Sambamba na hayo Nyambi ameongeza kuwa mikataba ya bei ya tumbaku wanaposaini wanakubaliana vitu vingi ikiwemo adhabu kwa wakulima ambao wanachafua tumbaku kiasi cha shilingi laki tano Pamoja na kutaifisha tumbaku za mkulima huyo.

“Tumeshakubaliana katika mikataba mtu akikakamatwa ameweka uchafu anaweza kutaifishwa tumbaku yake na mtu akikutwa amechanganya madaraja atatozwa faini ya shilingi laki tano,sasa isifike mahala tuanze kutafutana ili kumsaidia mkulima ambaye kaweka uchafu mwenyewe” Ameongeza Nyambi.
Kwa upande wake kiongozi wa bodi ya tumbaku mkoa wa kitumbaku Kahama Lukas Mihambo amesema kuwa swala la kususua kwa bei ya tumbaku msimu huu unatokana na vitendo vya wakulima kuweka uchafu kwenye tumbaku na kwamba semina hiyo inalenga kuwakumbusha wakulima wachambue vizuri tumbaku zao na amewataja wakulima wa Kata ya Bulungwa na Ulowa kuongoza katika vitendo hivyo.

“Msimu huu bei ya Tumbaku imechelewa kutoka kutokana na sisi wenyewe kuweka uchafu kwenye tumbaku zetu,kwahiyo tumekuja kuwakumbusha wakulima kuchambua tumbaku zetu vizuri na kufunga vizuri,Ulowa na Bulungwa mnaongoza kuweka uchafu sasa msimu huu msipokuwa makini tumbaku zenu zitataifishwa” Amesema Mihambo.
Naye afisa kilimo halmashauri ya Ushetu Given Ngilangwa ametoa wito kwa wakulima kuwa walinzi wenyewe kwa wenyewe kwa kuwafichua watu ambao wanatorosha tumbaku na kuuza holela mitaani na kwamba waepuka kuwabeba wakulima wasio na namba kwani wengi wao ndio wanaoweka uchafu.

“Tumbaku zinauzwa mchana kweupe mitaani na utakuta mkulima unamjua na unafahamu fika kufanya hivyo ni kosa ila mnakaa kimya,wafichueni watu wa namna hii lakini pia muwe makini na watu mnaowabeba kupitia namba zenu hawa wanaweza kusababisha tumbaku yako yote ikataifishwa” Amesisitiza Bi.Ngilangwa.
Msimu wa masoko ya Tumbaku unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 27 mwezi wa 4 ambapo kwa mkoa wa kitumbaku Kahama yatafanyika Mjini na vijijini.

Discussion
Reader comments
0 contributions