Na Adam Msafiri - Mara.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 198, na kuvuka lengo la makusanyo la Shilingi bilioni 192 lililowekwa kwa mwaka wa fedha, mafanikio yanayotajwa kuchangiwa na ongezeko la ulipaji wa kodi kwa hiari kutoka kwa walipa kodi.
Akizungumza katika Bonanza la Amani na maadhimisho ya miaka 30 ya TRA lililofanyika mjini Musoma, Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Masawa Masatu, amesema ushirikiano wa walipa kodi na wadau mbalimbali umewezesha mamlaka hiyo kufikia na kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato.

Masatu amewashukuru walipa kodi kwa kuendelea kutimiza wajibu wao bila kushurutishwa, akisema mapato hayo yanaendelea kuiwezesha Serikali kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amewataka wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanategemea mazingira salama na utulivu wa nchi.

Baadhi ya wakazi mkoani Mara pamoja na viongozi wa dini wametumia hafla hiyo kuwahimiza vijana kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya taifa, wakisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Bonanza hilo liliandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA, likiwa na lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari pamoja na kuendeleza ujumbe wa amani katika jamii.

Discussion
Reader comments
0 contributions