Na Ibrahim Rojala - Geita.
Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) imewafungia kibali wafanyabiashara watatu wa pembejeo za kilimo wilayani Geita baada ya kubainika kuuuza mbegu bila kibali na pasipo kuthibitishwa na TOSCI.
Mkuu wa TOSCI Kanda ya Ziwa, Ayub Mushema ameeleza kuwa hayo yamejiri kufuatia oparesheni maalum iliyofanyika mjini Geita yenye lengo la kudhibiti biashara ya pembejeo zisizo salama.
Mushema amesema katika oparesheni hiyo maduka hayo yamekutwa yakiuza mbegu zilizo nje ya muda wa miezi saba na zisizo halali kwa matumizi ya mkulima na hazikupaswa kusalia sokoni.

“Katika duka la Katumbi Agrovert tumebaini makosa mawili, kosa la kwanza ni kuuza mbegu bila kibali lakini kosa la pili tumekuta kuna baadhi ya mbegu ambazo zimeisha muda wake.
“Kwa hiyo kutokana na makosa haya mawili huyu mtu tumelazimika kumfungia kibali cha kuuza mbegu kwa sababu anauza mbegu kinyume na utaratibu,” amesema.
Alitaja mfanyabiashara mwingine aliyefungiwa kibali ni Msuka Agrovert ambaye alibainika kuuza mbegu ambazo zipo nje ya muda wa miezi saba huku kibali chake cha biashara kikiwa kimeisha.
“Lakini vilevile kuna duka la Ndaro Agrovert tumekuta mbegu ambazo hazina nembo na zipo nje ya muda wa matumizi” alifafanua Mushema.

Mushema amesema uchunguzi wa TOSCI umebaini pia yapo makampuni ambayo yanazalisha mbegu zake zikiwa hazijakidhi vigezo na hivo ufuatiliaji unaendelea kuwachukulia hatua.
“Kwa mjibu wa sheria ya mbegu inamtaka mzalishaji, msambazaji na mfanyabiashara wa mbegu kuhakikisha mbegu wanazosambaza ziwe ndani ya muda sahihi wa matumizi”, amesema.
Mkaguzi wa Mbegu Mwandamizi kutoka TOSCI Kanda ya Ziwa, Joseph Ngura amewaomba wakulima kufanya ukaguzi wa kina kabla ya kununua mbegu ili kuepuka kuuziwa mbegu feki.
Mmoja ya wauzaji wa pembejeo waliofungiwa, Mawazo Mwiga amesema changamoto kubwa inatokana na baadhi ya kampuni kukosa uaminifu na kuwasambazia mbegu zisizo na uhalali.
Discussion
Reader comments
0 contributions