Utafiti wa Wanasayansi wa NASA umelitaja Jiwe la anga (Meteorite) lenye rangi ya waridi lililopatikana Jangwa la Sahara mwaka 2022, kuwa ni kipande cha sayari ya Mirihi (Mars) chenye umri wa miaka Bilioni 4.1.
Taarifa ya NASA imedai kuwa Meteorite hiyo yenye uzito wa karibu paundi mbili, ilipatikana nchini Mali na ilipewa jina la Teghaza 001, kutokana na jina la tambarare ya chumvi, ilipopatikana.
Uchunguzi wa meteorite hiyo uliwaruhusu NASA kubaini kuwa ilikuwa moja kati ya meteorite takriban 435 zinazotoka Mirihi.

Meteorite zinaweza kuthibitishwa kama zilikuwa sehemu ya Mirihi kwa kulinganisha muundo wake wa kikemikali na madini na sampuli na data zilizokusanywa na misheni za NASA za Mirihi.
Upimaji wa umri wa meteorite hiyo uliwafanya watafiti kuhitimisha kuwa ilikuwa na umri wa takriban miaka bilioni 4.1, na kuifanya kuwa moja ya meteorite tatu za kale zaidi za Mirihi kuwahi kupatikana Duniani.
Hatua hiyo inatoa "mtazamo wa kipekee ya ukoko wa sayari hiyo na jinsi ilivyoundwa.

Picha ya karibu ya Teghaza 001, meteorite ya Mirihi.
Meteorite za kale za Mirihi zilizopita, zilitoa mwonekano finyu zaidi wa historia ya sayari hiyo, lakini Teghaza 001 inaonyesha jinsi ukoko wa Mirihi ulivyoundwa kutokana na magma iliyopoa na kisha kubadilishwa na maji yaliyokuwa kwenye uso wa sayari hiyo.
METEORITE ni nini?
1. Hili ni jiwe linalotoka angani, kwa mujibu wa Sayansi ni kwamba, angani kuna mawe mengi yanayoruka ruka - mengine ni mabaki ya sayari, mengine ni nyota zilizolipuka.

2. Jiwe likiwa bado angani linaitwa Meteoroid.
3. Likianza kuingia Duniani na kuwaka moto angani (ule mstari wa mwanga unaouona usiku watu wanasema "nyota imetoka") - linaitwa Meteor.
4. Lisiungue lote na likafanikiwa kuanguka chini ardhini, hilo jiwe sasa linaitwa Meteorite.
Hivyo, Meteorite ya Teghaza 001 ni jiwe lililotoka kwenye sayari ya Mars, likaruka angani kwa mamilioni ya miaka, likaangukia Jangwani mwa Sahara.

Hii ndiyo maana NASA wanasema ni kama Rosetta Stone, ni jiwe linalowaambia siri za jinsi sayari ya Mars ilivyoumbwa miaka Bilioni 4 iliyopita.
Discussion
Reader comments
0 contributions