Na Faustine Kasala - Kigoma.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ametoa maelekezo kwa Viongozi wa Shirika la uwakala wa Meli Tanzania TASAC na Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA kuhakikisha Mabaharia wa kike wanawezeshwa na kupewa kipaumbele katika kupata kazi melini sambamba na Kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia maslahi ya mabaharia hapa nchini.
Akifunga maadhimisho ya 16 ya Wiki ya Mabaharia yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Kigoma Prof. Mbarawa amesema, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya usafiri Majini ni lazima changamoto za Mabaharia zitatuliwe kwa wakati jambo ambalo linaenda sambamba na kuwawezesha mabaharia wa kike kupata kazi Melini.

"Napenda kutoa maelekezo manne siku ya leo kwa menejimenti ya TASAC na TPA. 1. Tasac walifanyie kazi suala la mabaharia kupata meli za kufanyia kazi. 2. Mabaharia wa kike wawezeshwe na kupewa kipaumbele katika kupata kazi melini. 3. Tuwe na Database ya mabaharia wetu wote walipo, na meli wanazofanyia kazi ndani na nje ya nchi. 4. Kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia maslahi ya mabaharia hapa nchini, kama ipo basi iboreshwe na kupewa nguvu," aliongeza Prof. Makame.
Aidha Prof! Makame amewahimiza Mabaharia kuwa wawazi na waaminifu katika shughuli zote ili kulinda usalama na uaminifu wa taaluma yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kuhusu chombo cha usafiri na kwa wakati ili kurahisisha uokoaji wakati wa dharura.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha Mabaharia Tanzania TASU Captein Josiah Mwakibuja amesema wanatambua juhudi za serikali katika kuendeleza na kuimarisha Miundombinu ya usafiri majini ikiwemo kupatikana kwa meli ya Uvuvi ya Taifa, kuanza kwa Safari ya Meli ya Mapinduzi kati ya Unguja na Pemba hatua ambayo imeongeza Fursa za ajira nchini.

"Pamoja na Mafanikio hayo ndg Mgeni Rasmi tunaomba Serikali kukamilisha kwa haraka sera mtambuka ya usafirishaji majini kwani kukamilika kwa Sera hiyo kutasaidia kuwa na Dira ya Pamoja ya maendeleo ya Sekta, kuvutia wawekezaji,uratibu bora wa Taasisi, kuimarisha mchango wa Serikali katika uchumi wa Buluu pamoja na kuongeza ushindani wa Sekta," alisema Captain Mwakibuja.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dr Rashid Chuachu akizungumza kwa niamba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro amesema uwekezaji katika sekta ya uchukuzi unaofanywa na Serikali Mkoani Kigoma unadhihirisha kwa vitendo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuufungua mkoa wa Kigoma.

"Rais Samia katika Ziara yake hapa Mkoani Kigoma alisema ataufungua Mkoa wa Kigoma na sasa tunashuhudia uwekezaji unaoendelea ni wa hali ya juu Mfano! Maboresho ya uwanja wa ndege,Ukarabati wa Meli ya Mv Liemba,ununuzi wa boti na utekeleza wa mradi wa Tren ya kisasa SGR haya ni baadhi tu ambayo yanadhihirisha dhamira ya Rais wetu kutaka kuufungua mkoa wa Kigoma Kiuchumi," alisema Dkt. Rashid.
Maadhimisho ya wiki ya Mabaharia Kitaifa yalizinduliwa Rasmi 22June 2026 mkoani Kigoma katika viwanja vya Mwanga Community Center na kufungwa rasmi June 25-2026 ambapo kwa mwaka huu yamebebwa na Kauli mbiu isemayo "Kutoka Sera hadi utekelezaji kuimarisha ubora katika sekta ya usafiri majini.
Discussion
Reader comments
0 contributions