Serikali imeiwezesha Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupata Dola za Marekani Milioni 65 kwa ajili ya utekelezaji wa matengenezo ya miundombinu ya barabara kupitia Mfuko wa Dharura wa Urejeshaji wa Miundombinu (CERC).
Akiwa mkoani Tabora, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, akiambatana na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya wakala huo, amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Ndevelwa lenye urefu wa mita 22 pamoja na barabara zake za maingilio zenye urefu wa mita 290 katika barabara ya Ndevelwa yenye urefu wa kilomita 20.2 iliyopo Manispaa ya Tabora.

Mhandisi Seff amesema fedha hizo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia uliotolewa kufuatia tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua za El-Nino za mwaka 2024, ambazo zilisababisha athari kubwa katika barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema "utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kurejesha na kuboresha miundombinu iliyoharibiwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji kwa urahisi, huku shughuli za kiuchumi na kijamii zikiendelea bila vikwazo vinavyotokana na ubovu wa barabara."

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora amesema ujenzi wa daraja la Ndevelwa umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kuimarisha mawasiliano kati ya kata na vijiji vinavyotegemea barabara hiyo, hasa wakati wa msimu wa mvua ambapo usafiri ulikuwa ukitatizika kutokana na mafuriko.
"Fedha hizi za CERC zinatoa fursa muhimu ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na majanga ya asili kwa haraka. Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kupitia fedha hizi inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi wapate huduma bora na salama za usafiri," amesema Mhandisi Seff.


Discussion
Reader comments
0 contributions