Tanzania leo, Novemba 5, 2026, itakuwa katika jukwaa la kimataifa la haki za binadamu jijini Geneva, itakapowasilisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizotekelezwa katika kuimarisha utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na ustawi wa wananchi, katika Mapitio ya Nne ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Ushiriki huo unaipa Tanzania fursa ya kueleza mbele ya jumuiya ya kimataifa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mapitio yaliyopita, hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na maeneo yanayoendelea kupewa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, amesema Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia falsafa ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs).

Amesema mapitio hayo ni fursa muhimu kwa Tanzania kueleza mafanikio yaliyopatikana, hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo yaliyokubaliwa katika duru zilizopita, pamoja na kuonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha haki za binadamu na ustawi wa wananchi.
Tanzania inashiriki katika duru ya nne ya UPR ikiwa tayari imeshiriki katika mapitio matatu yaliyotangulia mwaka 2011, 2016 na 2021.
Katika duru ya tatu, iliyofanyika mwaka 2021, nchi ilipokea mapendekezo 252 kutoka kwa mataifa mbalimbali, ambapo iliridhia mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku 65 yakikosa kuridhiwa.
Discussion
Reader comments
0 contributions