Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania iko tayari kwa AFCON 2027, baada ya kukagua miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Ziwa Duluti, Arusha, na kuhakikishiwa kuwa ujenzi wa baadhi ya miundombinu hiyo umefikia asilimia 95.
Dkt. Kijaji alitoa kauli hiyo Oktoba 24, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya shughuli za utalii na ujenzi wa miundombinu katika hifadhi hiyo. Arusha ni miongoni mwa majiji yatakayotumika katika mashindano hayo yatakayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

Katika maandalizi ya michuano hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii ina jukumu la kuratibu huduma za malazi na chakula kwa wageni, pamoja na kuhakikisha wanapata huduma bora za ukarimu wakati wa mashindano hayo.
Akizungumzia maandalizi ya TFS, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi Saidizi ya Utawala, Emmanuel Kiboko, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, alisema wakala huo unalenga kutumia fursa ya AFCON 2027 kuongeza mapato yatokanayo na utalii katika Hifadhi ya Ziwa Duluti.
Kiboko alisema TFS, kwa kushirikiana na wadau, imewekeza katika nyumba 20 za kulala wageni (cottages) na mahema ya kifahari (executive tents) ili kuongeza uwezo wa hifadhi hiyo kutoa huduma za malazi kwa watalii na wageni.

Alisema uwekezaji huo unalenga kuboresha huduma za utalii na kuongeza mapato wakati wa mashindano na baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji alikagua ujenzi wa nyumba za kulala wageni na miundombinu ya shughuli za burudani, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miundombinu hiyo inazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu.

Aliwahimiza Watanzania na wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo katika hifadhi za misitu kuwekeza kwenye utalii, akisema bado kuna maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji, ikiwemo Ziwa Duluti. Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira.
Discussion
Reader comments
0 contributions