Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise, amesema mvua za mara kwa mara zinazoikumba Kagera zinaweza kuchelewesha maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo kutegemea zaidi msimu wa kiangazi.
Mbise amesema endapo mvua zitakuwa nyingi na zaidi ya kiwango cha wastani, maendeleo ya baadhi ya miradi yanaweza kuathirika, lakini hali hiyo haitazuia barabara na maeneo mbalimbali kupitika, huku wakandarasi wakielekezwa kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kutumika wakati wote.

Amesema TANROADS imewaelekeza wakandarasi wanaotekeleza miradi mikubwa mkoani Kagera kuhakikisha barabara zinapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa El Nino, huku akiwataka wananchi kutokuwa na hofu kuhusu kukamilika kwa miradi hiyo, kwa kuwa mipango imewekwa kuhakikisha inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.
Mbise ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TANROADS Mkoa wa Kagera zilizopo Manispaa ya Bukoba, wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya taasisi hiyo kuelekea msimu wa mvua za El Nino, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
"Hadi sasa TANROADS Mkoa wa Kagera imekamilisha taratibu za kuwapata takribani asilimia 50 ya wakandarasi wanaohitajika kwa ajili ya matengenezo ya barabara, ambapo baadhi yao tayari wameanza kuzibua mitaro na kalavati ili kuwezesha maji ya mvua kupita kwa urahisi na kupunguza uwezekano wa kuziba kwa njia hizo na kusababisha uharibifu wa barabara"
Mbise ameongeza kuwa wakandarasi watano wenye uwezo mkubwa wameandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua, huku vifaa vya dharura vikiwemo kalavati za chuma zenye urefu wa mita 600, kalavati za plastiki zenye urefu wa mita 160 na waya wa gabioni wenye ujazo wa mita 1,080 vikiwa tayari kwa matumizi.

Aidha, vifaa hivyo vitatumika katika maeneo yatakayohitaji hatua za haraka, ambapo waya wa gabioni hutumika kutengeneza miundo ya gabioni inayojazwa mawe kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuvunjika kwa barabara hususan katika maeneo ya madaraja na kalavati.

Hivyo, TANROADS imefanya tathmini ya maeneo hatarishi yanayoweza kuathiriwa na mafuriko na kuyaweka katika ufuatiliaji wa karibu kupitia wakaguzi wa barabara, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa ofisi za TANROADS Mkoa wa Kagera au maafisa usalama barabarani pindi dharura itakapotokea, ili hatua za haraka zichukuliwe.
Discussion
Reader comments
0 contributions