Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele amesema kwa mwaka huu (2026) Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, wamekuja na maonesho tofauti yanayowapa wananchi fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za umeme.
Bi. Gowele ameyasema hayo Julai 04,2026 kwenye banda la shirika hilo wakati akizungumza na vyombo vya habari na kuongeza kuwa kivutio kikubwa ni Nyumba Janja (Smart Home), ambayo ina mfumo wa kisasa wa wiring ya kidijitali unaosaidia kuongeza usalama wa nyumba dhidi ya majanga kama moto pamoja na kuruhusu mmiliki kudhibiti matumizi ya vifaa vya umeme akiwa popote duniani kupitia simu ya mkononi.
“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ninawakaribisha wananchi wote na wateja wetu kutembelea banda letu. Mbali na uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, mwaka huu tunawaonesha Watanzania thamani ya matumizi ya umeme katika maisha yao ya kila siku,” alisema Gowele.

Kwa mujibu wa Gowele, amesema mfumo huo humwezesha mtumiaji kuwasha au kuzima vifaa vya umeme kwa kutumia programu maalumu na kufuatilia kiwango cha umeme kinachotumiwa na kila kifaa, hatua inayosaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Aidha, amesema TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi (energy efficient), huku nyumba hiyo ikiwa imewekewa vifaa vinavyotumia kiwango kidogo cha umeme ili kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za matumizi.
Gowele pia amewakumbusha wananchi kuhusu mpango wa TANESCO wa kukopesha majiko ya umeme, akisema wanaotembelea banda hilo wanaweza kuyapata kwa kununua au kwa mkopo kwa kutumia namba ya mita na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kwa ajili ya uhakiki.
"Majiko haya ni ya matumizi yenye ufanisi mkubwa na yana uwezo wa kupika chakula cha Kitanzania kwa umeme wenye thamani ya chini ya shilingi 356, hivyo kuwa mbadala nafuu wa nishati nyingine za kupikia,"amesema.
Katika maonesho hayo, wananchi pia wanapata fursa ya kujionea kwa teknolojia ya kidijitali miradi mikubwa ya TANESCO, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu mkoani Shinyanga unaozalisha megawati 50.
Pia amesema banda hilo linaelimisha wananchi kuhusu matumizi ya umeme katika sekta ya usafiri kupitia magari, pikipiki na bajaji zinazotumia umeme, akisisitiza kuwa Tanzania ina umeme wa kutosha hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kupunguza gharama za usafiri na kulinda mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Discussion
Reader comments
0 contributions