Wadau na wamiliki wa viwanda mkoani Singida wamepata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili katika matumizi ya huduma za umeme, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likiweka mpango wa kuanzisha vituo vidogo vya huduma katika kila wilaya nchini ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Ben Krumba, Afisa Mahusiano na Wateja Wakubwa, mbele ya Kaimu Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Joanfeith Tarahiya, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, katika hafla iliyofanyika mjini Singida.
Akizungumza katika hafla hiyo, Krumba amesema TANESCO imeendelea kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma, ikiwemo kutengeneza mfumo maalumu wa kuhudumia wateja wakubwa wa shirika pamoja na kuimarisha huduma kwa wateja wanaotekeleza majukumu yao kwa wakati. Hafla hiyo imewakutanisha wadau pamoja na wamiliki wa viwanda kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida, waliopata ufafanuzi na ufumbuzi wa changamoto zao kutoka TANESCO.
Katika hafla hiyo, TANESCO Mkoa wa Singida imekabidhiwa tuzo ya kitaifa kwa kutambua utendaji wake katika kuhudumia wateja wakubwa na wateja binafsi. Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za shirika hilo za kuboresha huduma, kuwasikiliza wateja na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa ufanisi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.
Discussion
Reader comments
0 contributions