Na Hadija Omary - Lindi.
Wananchi 1,730 wanaopisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme wenye msongo wa kV 220 kutoka Masasi hadi Mahumbika wameanza kulipwa fidia zao na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Lindi. Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa zoezi la uthamini wa mali za wananchi lililofanyika mwezi Machi 2026.
Zoezi la malipo kwa Wilaya ya Lindi limeanza rasmi Aprili 7, 2026, katika vijiji viwili vya Kiwalala na Mahumbika. Katika siku ya kwanza, wanufaika takribani 78 wamelipwa fedha zao moja kwa moja, huku wakieleza furaha yao kwa Serikali kutimiza ahadi yake kwa wakati.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja Kitengo cha Mazingira kutoka TANESCO, Tula Isaba, alisema kuwa kwa sasa malipo yameanza katika vijiji viwili kati ya vinne vya kata hiyo. Aliongeza kuwa wanatarajia kulipa jumla ya vijiji 14 vya Halmashauri ya Mtama kabla ya kuzifikia Wilaya za Ruangwa, Newala na Masasi zilizopo kwenye mkondo wa mradi huo.
Zoezi hilo muhimu limeshuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, pamoja na viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya na Chama. Viongozi hao waliwataka wananchi waliolipwa kutumia fedha hizo kwa manufaa, kwa kujenga nyumba bora, kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi na kuinua kipato cha familia zao badala ya kuzitumia kwa anasa.

Mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 220 kutoka Masasi hadi Mahumbika unatarajiwa kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme Mkoa wa Lindi na kusini mwa Tanzania kwa ujumla, pamoja na kuchochea uwekezaji katika viwanda na kilimo cha kisasa mara utakapokamilika.



Discussion
Reader comments
0 contributions