Serikali imekabidhi gari aina ya Isuzu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, kwa lengo la kurahisisha na kuimarisha utoaji wa huduma za umeme kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Akizindua gari hilo katika Kata ya Loya, Wilaya ya Uyui, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mohamed Mtulyakwaku, ameishukuru Serikali kwa kutoa gari hilo, akieleza kuwa litasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Pia amewahimiza wananchi kutumia vyema fursa mbalimbali zinazotokana na upatikanaji wa nishati ya umeme kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Uyui, Hamid Kionywaki, amesema gari hilo litaongeza kasi ya kuwahudumia wananchi, hususan katika matengenezo ya miundombinu ya umeme na utekelezaji wa miradi ya kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo huku akiongeza kuwa Wilaya ya Uyui ina vijiji 156 ambavyo vyote vimefikiwa na huduma ya umeme.

Aidha, TANESCO inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 706 vya wilaya hiyo, ambapo hadi sasa asilimia 32 ya vitongoji hivyo tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme kwa ajili ya kuchochea maendeleo na kuboresha maisha yao.


Discussion
Reader comments
0 contributions