Na Clavery Christian - Kagera.
Serikali mkoani Kagera imekabidhi jumla ya vyombo vya moto 29 kwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoa wa Kagera, ikiwa ni jitihada za kuimarisha huduma za umeme kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa shirika hilo.
Vyombo hivyo vinajumuisha magari manne, pikipiki za miguu miwili pamoja na pikipiki za miguu mitatu, ambavyo vimekabidhiwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Kanali Kido alisema kuwa serikali imeamua kuwekeza katika vitendea kazi hivyo ili kusaidia mafundi na watumishi wa TANESCO kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi pale panapotokea hitilafu za umeme.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya uhakika na inayopatikana kwa wakati. Vyombo hivi vitasaidia sana katika kushughulikia changamoto za kiufundi kwa haraka, hasa katika maeneo ya vijijini,” alisema mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Kido.

Alisisitiza kuwa watumishi wa TANESCO wanapaswa kuvitumia vyombo hivyo kwa uangalifu na kuwajibika ili kuhakikisha vinadumu na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Naye meneja wa TANESCO mkoa wa Kagera alieleza kuwa upatikanaji wa vyombo hivyo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili, hususani wakati wa kushughulikia dharura za kukatika kwa umeme.

Aliongeza kuwa sasa wataweza kuwafikia wateja kwa wakati, kufanya matengenezo kwa haraka na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa huo.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya nishati nchini, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ya uhakika ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Discussion
Reader comments
0 contributions