Na Eunice kanumba – Kishapu.
Tamasha la utamaduni linalowakutanisha koo ya kabila la wasukuma waliokuwa chini ya utawala wa Mwanamama NSIYA kabla ya kuja kwa ukoloni maarufu kama Sanjo ya Busiya limefanyika katika Kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, na kuhudhuriwa na mamia ya watu hususani kutoka katika koo hiyo ili kuendeleza utamaduni, mila na desturi zao.
Akizungumza katika tamasha hilo mtawala wa Tatu wa Sanjo hiyo Faustine Makani anayejulikana kama Chief Makwaia wa tatu ametoa wito kwa wananchi kuendeleza utamaduni, mila na desturi zao, pamoja na kudumisha upendo na amani ya nchi.

Amesema, tamasha hilo la Sanjo ya Busiya ni la kumi na sita, na limekuwa nyenzo muhimu ya utamaduni kwa wana-Busiya na wananchi wa ujumla, ambalo linasisitiza upendo na kuwa wamoja.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mboni Mhita, amelipongeza tamasha hilo la utamaduni ambalo limekuwa likiwaunganisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali kusherehekea kwa pamoja na kuonyesha Tanzania ni nchi ya amani.

“Tamasha hili la utamaduni limeunganisha watu wengi na kuonyesha kuwa sisi ni damu moja na Watanzania wamoja. hivyo, tushirikiane katika kufanya kazi na kudumisha amani ya nchi yetu,” amesema Masindi.
Nao baadhi ya wananchi wa Kishapu, akiwamo Bugali Mbushi, wameeleza kuwa tamasha hilo limekuwa likiwajenga kuwa wamoja na kuendeleza mila na desturi zao,ambapo Tamasha hilo limehudhuriwa na machifu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwamo nchi za Kenya na Afrika Kusini.

Kabla ya kuwasili kwa wakoloni Busiya Chiefdom ilikuwa miongoni mwa tawala za jadi zilizokuwa na nguvu mchango mkubwa katika uongozi wa jamii za wenyeji. Utawala huo uliongozwa na chifu NSIYA aliyesimamia masuala ya utawala, usalama, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa rasilimali za jamii kwa kushirikiana na wazee wa kimila.
Busiya Chiefdom pia ilikuwa kitovu cha kuhifadhi mila, desturi na utamaduni wa jamii, huku viongozi wa jadi wakihakikisha amani, mshikamano na maendeleo ya wananchi kupitia mifumo ya jadi ya utawala. Uchumi wa eneo hilo ulitegemea kilimo, ufugaji na biashara ya kubadilishana bidhaa kati ya jamii jirani.

Hata hivyo, ujio wa utawala wa kikoloni ulisababisha mabadiliko makubwa katika mfumo wa uongozi wa jadi, ambapo mamlaka ya machifu yalipunguzwa au kuingizwa katika mfumo mpya wa utawala wa kikoloni. Licha ya mabadiliko hayo, historia ya Busiya Chiefdom inaendelea kutambuliwa kama sehemu muhimu ya urithi wa kihistoria na utamaduni wa jamii za eneo hilo.

Discussion
Reader comments
0 contributions