Wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Tamasha la Buha 2026, jukwaa linalolenga kuimarisha mahusiano, ushirikiano na mshikamano wa jamii, pamoja na kuenzi na kuendeleza urithi wa Waha.
Tamasha hilo limeandaliwa na Umoja wa Ibhuha Yachu, likiwa na lengo la kuwakutanisha Waha wanaoishi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania na nje ya nchi, kwa ajili ya kuenzi urithi wa Buha, kujenga mshikamano na kujadili namna ya kushirikiana katika kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Kigoma kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Buha 2026, Stewart Ernest Zindutse, amesema urithi wa Buha ni sehemu muhimu ya utajiri wa utamaduni wa Tanzania, hivyo tamasha hilo litakuwa jukwaa la kutangaza na kuendeleza lugha, historia, mila na desturi za Waha.

Viongozi mbalimbali wakizungumza na wanahabari Kigoma kuelekea TAMASHA LA BUHA 2026, (Picha na Tryphone Odace)
Alisema lengo ni kuhakikisha urithi huo unaendelea kuhifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, huku vijana wakipewa nafasi ya kuufahamu na kuuthamini.
Kwa upande wake, Dkt. Peter Mayengo, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, amesema pamoja na kuenzi na kutangaza urithi wa utamaduni wa Buha, vijana watapata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya teknolojia katika kujiajiri na kuongeza kipato.
Amesema teknolojia inaweza kuwa nyenzo muhimu kwa vijana katika kutafuta fursa za kiuchumi, kukuza vipaji na kutangaza bidhaa na huduma zao kwa kutumia majukwaa ya kidijitali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Mawasiliano wa Umoja wa Buha Yetu, Prosper Kwigize, alisema tamasha hilo pia litatoa nafasi kwa wananchi wa Kigoma kupata elimu ya uraia na uzalendo.
Alisema elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa kuhusu wajibu wao katika jamii na umuhimu wa kushiriki katika shughuli zinazolenga kuimarisha maendeleo na mshikamano wa taifa.
Aidha, tamasha hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa wajasiriamali, vikundi vya wanawake na vijana, wasanii, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuonyesha bidhaa, huduma, vipaji na kazi zao.
Tamasha la Buha 2026 linatajwa kuwa na umuhimu katika kuunganisha utamaduni na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kupitia tamasha hilo, Waha kutoka ndani na nje ya Tanzania watapata nafasi ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kutumia umoja wao katika kuchochea maendeleo ya Kigoma.
Pia, tamasha linaweza kutoa nafasi kwa Mkoa wa Kigoma kutangaza utamaduni wake, vipaji, bidhaa za wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazopatikana mkoani humo.
Kwa upande wa vijana na wanawake, jukwaa hilo linatoa fursa ya kuonekana kwa kazi zao, kujenga mitandao ya kibiashara, kujifunza kutoka kwa wadau mbalimbali na kutafuta fursa zinazoweza kuongeza kipato.
Waandaaji waliwahimiza Waha wanaoishi Tanzania na nje ya Tanzania, wasanii, wanazuoni, wajasiriamali, taasisi binafsi na za umma pamoja na wananchi wengine kushiriki katika tamasha hilo.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya kukutana kwa watu wenye asili ya Buha, kujifunza kuhusu historia na utamaduni wao, kujenga mahusiano na kuibua mijadala na fursa zinazoweza kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Kigoma.
Tamasha la Buha 2026 linatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 17 hadi 19, 2026, likiwa na kaulimbiu: “Tukumbuke Asili, Tujenge Umoja na Maendeleo.”
Discussion
Reader comments
0 contributions