Na Saulo Stephen – Singida.
Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida umefanikisha kurejeshwa kwa betri nne za mita za maji za malipo ya awali (Prepaid Water Meters Batteries) zenye thamani ya shilingi milioni 6.5, zilizokuwa hazijawasilishwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) tangu zilipopokelewa mwaka 2023.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi wa SUWASA, Christopher Anthony Kenyunko, alipokea betri hizo kutoka kwa mzabuni mwaka 2023 lakini hakuzifikisha SUWASA kama ilivyotakiwa. Baada ya uchunguzi kukamilika, suala hilo lilipelekwa mahakamani ambapo mshtakiwa alikiri kosa na kuahidi kuzirejesha betri hizo.

Betri hizo zimekabidhiwa rasmi katika Ofisi za SUWASA Mkoa wa Singida mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Bw. Hosea Julius Mghimbi, wataalamu watatu wa taasisi hiyo waliothibitisha ubora na uhalali wa vifaa hivyo pamoja na maafisa wa TAKUKURU waliosimamia mchakato wa urejeshwaji.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Bw. Hosea Julius Mghimbi, aliishukuru TAKUKURU kwa kazi yake ya kulinda mali za umma na kuhakikisha vifaa hivyo vinarejeshwa kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Alisema kurejeshwa kwa betri hizo kutasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za maji kupitia mita za malipo ya awali na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Mkoa wa Singida.
Mghimbi pia aliwataka watumishi wa umma kuzingatia uadilifu katika usimamizi wa mali za serikali, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu.

"Taasisi hii ya TAKUKURU naipongeza kwa kazi kubwa walioifanya kuhakikisha betri hizi zinarudi na kuendelea kuhudumia wananchi. Pia natoa wito kwa wananchi kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa. Lazima tuelewe kwamba kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; sote tutimize wajibu wetu. Vilevile, watumishi wa umma wanapaswa kuwa waadilifu katika usimamizi wa mali za umma ili fedha za Serikali zitumike kwa manufaa yaliyokusudiwa," amesema Mghimbi.
Discussion
Reader comments
0 contributions