Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeipongeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), kwa juhudi za mapambano ya kuzia rushwa katika wilaya hiyo yenye halmashauri tatu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda wakati akifungua semina ya walimu walezi wa klabu za kupinga rushwa katika shule za sekondari kutoka manispaa ya Kahama,halmashauri ya Ushetu na halmashauri ya msalala.

Nkinda amesema kuwa TAKUKURU Wilayani Kahama wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia na kupambana na rushwa na kwamba wilaya ya Kahama kesi za rushwa zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za takukuru ikiwemo kutoa elimu kwa jamii.
“Niwapongeze sana TAKUKURU kwakweli kazi mnayofanya ni kubwa sana katika mapambano haya dhidi ya rushwa na tangu mimi nimefika Kahama malalamiko ya rushwa yamepungua kwa kiasi kikubwa” Amesema Nkinda.

Sambamba na hayo Nkinda amewataka walimu walezi wanaosimamia klabu za kupinga rushwa katika shule za sekondari wilayani Kahama kuendeleza na kuzisimamia klabu hizo ili kuwafundisha vijana uzalendo wa nchi yao na maadili ya kuchukia rushwa katika jamii.
“Klabu hizi zinasaidia sana vijana wetu kufahamu madhara ya rushwa wakiwa bado wadogo,kwahiyo rai yangu kwa walimu walezi wote endeleni kusimia klabu hizi ili watoto wetu wawe wazalendo katka nchi yao na waichukie rushwa tangu wakiwa wadogo,” amesema Nkinda.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Kahama Abdallah Urari amesema kuwa wamefungua klabu za wapinga rushwa katika vyuo vyote Kahama na shule za sekondari na kwamba wataendelea kufungua klabu hizo katika shule zote za msingi wilaya ya Kahama.
“Kwa sasa wilayani kahama klabu za wapinga rushwa zimefunguliwa katika shule za sekondari na vyuo,na tunaendelea kufungua klabu hizi katika ngazi ya shule za msingi katika manispaa ya Kahama,Ushetu na Msalala kulingana na muongozo uliotolewa,” amesema Urari.

Kwa upande wao baaadhi ya walimu walezi Lubango Joseph kutoka shule ya sekondari kishimba na Fatuma kidubo kutoka shule ya sekondari Nyahanga wamesema kuwa wamefurahi kupata mafunzo hayo kwani walikuwa wanaendesha klabu hizo bila mafunzo yoyote na kwamba klabu hizo zitawasaidia wanafunzi kujua madhara ya rushwa na kuwa mabalozi katika jamii.
“Tunashukuru sana kwa kupata mafunzo haya sisi kama walezi wa klabu hizi tulikuwa tunaendesha klabu hizi bila semina ila kwasasa tunaenda kufufa klabu hizi kwani zinawasaidia wanafunzi kupata uelewa kuhusu madhara ya rushwa,” walisema Walimu hao.

Naye mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya sekondari Cherehani iliyopo Bugomba B halmashauri ya Ushetu, Justine Majogolo amesema kuwa kuanzishwa kwa klabu hizo zitawajengea uwezo wanafunzi kuijua rushwa wakiwa shuleni na kuiomba TAKUKURU kuanzisha klabu hizi katika shule zote hususan zilizopo vijijini.
“Kwakweli klabu hizi zimetusaidia sana sisi wanafunzi,tumepata uelewa mkubwa kuhusu madhara ya rushwa kwenye jamii,kikubwa tuombe TAKUKURU itoe elimu na kuongeza klabu katika shule za vijijini ili hii elimu ifike kwa kila mtu” Amesema Majogolo.
Discussion
Reader comments
0 contributions