Skip to main content

TAKUKURU KATAVI YAWATAKA WADAU KUSIMAMIA MIRADI KWA UADILIFU, UZALENDO

Na Daniel Gahu - Katavi.

TAKUKURU KATAVI YAWATAKA WADAU KUSIMAMIA MIRADI KWA UADILIFU, UZALENDO

Na Daniel Gahu - Katavi.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi imewataka wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kufanya kazi kwa uadilifu, uzalendo, uwazi na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo Juni 30,2026 katika warsha ya wadau wa usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Katavi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaji Majid Mwanga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko. Amesema warsha hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi na kutimiza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rai yetu kama mkoa ni kuhakikisha kila mmoja anatumia fursa hii kama nyongeza na chachu ya kufanya kazi kwa uadilifu ili dhamira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yafikiwe kwa wakati,” amesema Mwanga.

Amesema maeneo yenye vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka husababisha utekelezaji wa miradi kusuasua, hivyo amewataka washiriki kutumia maarifa watakayopata katika warsha hiyo kuziba mianya yote ya rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi.

Aidha, amesisitiza watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na kuwa mabalozi wazuri wa kuijenga nchi kupitia usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Bi. Sipha Mwanjala, amesema Serikali imeendelea kuwekeza rasilimali nyingi katika programu na miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.

“Rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo husababisha hasara kubwa kwa Serikali na jamii kwa ujumla kwa kuchochea ujenzi wa miradi isiyo na viwango, kuongeza gharama zisizo za lazima, kuchelewesha utekelezaji wa miradi na wakati mwingine kukwamisha huduma zilizokusudiwa kuwafikia wananchi,” amesema Bi. Sipha Mwanjala.

Ameongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni msingi muhimu wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta tija, kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali na kufanikisha maendeleo endelevu nchini.

Katika warsha hiyo TAKUKURU imehoji "Kwanini bado Kuna mianya na mapungufu katika mifumo(Miradi) licha ya kuwapo kwa mifumo ya udhibiti katika idara/taasisi zetu za umma?".

Ambapo wadau wa warsha hiyo wamelijibia swali hilo kwa kubainisha sababu za mapungufu hayo ni uzembe kwa baadhi ya wasimamizi na watekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo unakuta watu wanatamani vitu vizuri, watu wanatamani suti nzuri, magari mazuri, nyumba nzuri na vinginevyo jambo ambalo linapelekea watumishi wengi kuwa wajanjawajanja.

"TAKUKURU ni taasisi ambayo tunaitegemea sana hivyo binafsi niiombe iongeze juhudi zaidi za kuwafuatilia wahalifu na wabadhilifu wa Mali za Umma. Kama umefuga kuku na unataka kumkamata wakumchinja, huwa tunachukua mahindi tunatupia halafu tunawakamata,"

"kwa hiyo TAKUKURU endeleeni kutumia mbinu hiyo hiyo ambayo mnaitumia kuwakamata wabadhilifu na watumishi wote wenye tamaa kwa mali za Umma" amesema Onesmo Buswelu Mkuu wa wilaya ya Tanganyika ambaye pia ni mdau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali."

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.