Na Faustine Kasala - Kigoma.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma imepokea na kufanya uchunguzi wa malalamiko 221 yaliyotolewa na wananchi katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2026.
Akizungumza na wanahabari Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Elibaliki Kihundrwa, amesema kuwa kati ya malalamiko hayo 12 yamethibitika kuwa ni makosa ya Rushwa huku malalamiko 7 yakibainika kutohusiana na rushwa.
"Tumepokea malalamiko 221 kwa mwaka huu. Kesi 12 tumethibitisha kuwa zinahusiana na Rushwa na zinaendelea kuchukuliwa hatua. Malalamiko mengine tumeyaelekeza sehemu husika kwa utatuzi," alisema Kihundrwa.

Aidha Bw! Kihundrwa amesema tuhuma zinazojitokeza zaidi wilayani humo ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi ya umma.
"Matumizi mabaya ya madaraka ni tatizo kubwa. Baadhi ya watumishi wanatumia ofisi kujinufaisha. Tunawafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria," alisema Kihundrwa
Mkuu huyo wa TAKUKURU ameitaja Sekta ya Ardhi kuongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakikubali kutoa rushwa badala ya kudai haki zao.

"Ardhi ina malalamiko mengi. Wananchi waache tabia ya kuridhiana kutoa kitu. Huduma za ardhi ni bure kwa kufuata utaratibu toeni taarifa TAKUKURU tukomboe nchi," aliongeza Kihundrwa.
Aidha, TAKUKURU Wilaya ya Kasulu imewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za viashiria vya rushwa kwa namba ya bure 113 au kufika ofisini kwao kwa maslahi ya maendeleo endelevu katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Discussion
Reader comments
0 contributions