Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Gerald Mongella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, amezindua rasmi awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote katika Viwanja vya TBC, Manispaa ya Tabora.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, amesisitiza kuwa bima ya afya ni njia ya kulinda familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Ameeleza kuwa afya ni mtaji wa maendeleo, na kwamba utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 unahitaji viongozi kuhakikisha mpango huo unamfikia mwananchi wa kawaida.
Dkt. Momgella amesisitiza kuwa ufanisi wa mpango huo utategemea elimu sahihi na kuwafikia wananchi katika maeneo yao ya uzalishaji mali, ikiwemo masoko, vituo vya bodaboda, maeneo ya kilimo na vikundi vya kiuchumi.
Aidha Dkt. Mongela amewataka viongozi wa Serikali za mitaa, wadau na vyombo vya habari kushiriki katika uhamasishaji, huku vituo vya kutolea huduma vikiimarisha utayari wa kuwahudumia wanachama kwa mujibu wa mafao na masharti ya bima. 
Awali, Meneja wa NHIF Mkoa wa Tabora, Dkt. Raphael Malaba, amesema mpango huo ni mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za afya nchini na kuwataka wananchi kujitokeza kujiunga.
Ametoa wito kwa viongozi, watendaji wa Serikali za mitaa na wadau kuweka kipaumbele katika elimu na uhamasishaji ili walengwa wafikiwe na kunufaika na huduma za afya. 
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alisema changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zimekuwa fursa ya kujifunza na kuboresha utekelezaji wa awamu ya pili, huku akieleza kuwa Mkoa umejiandaa kikamilifu kutekeleza mpango huu muhimu wa awamu ya pili.
Uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupanua upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions