Wilaya ya Tabora imeanza kuchukua hatua za maandalizi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa ya El Niño.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha Kamati ya Maafa ya Wilaya kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Tabora.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazoweza kuambatana na hali ya hewa ya El Niño.
Akiongoza kikao hicho, DC Wella amezielekeza taasisi zinazounda Kamati ya Maafa ya Wilaya kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake kujiandaa mapema kwa kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Aidha, Wella amezielekeza taasisi hizo kukutana na kuandaa mpango mkakati wa pamoja wa namna ya kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotabiriwa.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, maandalizi ya mapema na uwajibikaji wa kila taasisi ili kuhakikisha Wilaya ya Tabora inakuwa tayari kukabiliana na athari za El Niño na kulinda usalama wa wananchi pamoja na mali zao.

Discussion
Reader comments
0 contributions