Na Adam Msafiri - Mara.
Baadhi ya watumishi wa umma mkoani Mara wameonywa kuacha tabia ya kujipatia malipo ya safari na posho za ukaguzi na usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa kutumia taarifa za uongo, huku wakiwa hawajafika katika maeneo husika ya miradi.
Onyo hilo limetolewa Julai 13,2026 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara, Mohamed Sharif, wakati wa warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoani humo.

Sharif amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakiwasilisha taarifa zisizo za kweli kwa wakuu wao wakidai walifanya ziara za kukagua na kusimamia miradi ya maendeleo, ilhali ukaguzi huo haujawahi kufanyika. Amesema tabia hiyo inachangia matumizi mabaya ya fedha za umma na kudhoofisha juhudi za Serikali za kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Wakili Restuta Kessy, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, uwajibikaji na sheria katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa kila mtumishi wa umma ana wajibu wa kulinda rasilimali za Serikali na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwepo ufuatiliaji wa karibu.

Akifunga warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameitaka TAKUKURU kuendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watumishi na viongozi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma. Amesisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa maslahi binafsi.
Wakati huo huo, baadhi ya washiriki wa warsha hiyo, wakiwemo viongozi wa dini, wameitaka jamii, hususan watu waliokabidhiwa dhamana za uongozi na usimamizi wa rasilimali za umma, kuwa waadilifu, kuwa na hofu ya Mungu na kujiepusha na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wao, viongozi mbalimbali walioshiriki warsha hiyo, wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya, wameahidi kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hadi ikamilike kwa wakati, pamoja na kukemea na kuchukua hatua dhidi ya viashiria vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za umma.

Discussion
Reader comments
0 contributions