Muigizaji wa Marekani, RJ Mitte, aliyefahamika zaidi kwa kucheza nafasi ya Walter White Jr. katika tamthilia maarufu ya Breaking Bad, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 34.
Taarifa za kifo chake zilitolewa na mwakilishi wake, Sean Reilly, aliyesema kuwa familia, marafiki na watu waliomfahamu wamepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kuondokewa na muigizaji huyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na BBC, Mitte alifariki katika eneo la Brownsville, jimbo la Texas, Marekani.
Hata hivyo, chanzo cha kifo chake hakikuwa kimetajwa wakati taarifa hiyo ilipotolewa, huku polisi wakisema kuwa uchunguzi kuhusu mazingira ya kifo chake ulikuwa unaendelea. Taarifa zilisema alitangazwa kufariki Oktoba 12, 2026.

Mitte alipata umaarufu mkubwa kupitia tamthilia ya Breaking Bad, iliyoonyeshwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2013. Katika tamthilia hiyo, alicheza nafasi ya Walter White Jr., mtoto wa Walter White, mhusika mkuu aliyechezwa na Bryan Cranston.
Uhusika wake ulimfanya ajulikane kwa watazamaji wengi kutokana na namna alivyoweza kuwasilisha maisha ya kijana anayekabiliana na changamoto za kifamilia huku baba yake akiingia katika ulimwengu wa uhalifu.
Mitte alikuwa akiishi na hali ya kiafya inayojulikana kama cerebral palsy, inayoathiri mwendo na uratibu wa misuli.
Uzoefu wake binafsi ulimsaidia kuwasilisha uhusika wake kwa uhalisia, huku nje ya uigizaji akijitolea kupigania haki, ushirikishwaji na uwakilishi bora wa watu wenye ulemavu katika tasnia ya filamu na jamii kwa ujumla.

Mbali na mafanikio yake katika Breaking Bad, Mitte alishiriki katika miradi mingine ya televisheni na filamu, ikiwemo Hannah Montana na Switched at Birth.
Pia alifanya kazi za kijamii kupitia taasisi na mipango iliyolenga kuhamasisha jamii kuhusu watu wenye ulemavu na kupinga mitazamo hasi dhidi yao.
Kifo chake kimeacha huzuni miongoni mwa waigizaji wenzake. Bryan Cranston, aliyeigiza kama baba yake katika Breaking Bad, alieleza kusikitishwa kwake na kifo hicho, akimkumbuka Mitte kama kijana aliyekua kutoka mwigizaji chipukizi hadi kuwa msanii mwenye uwezo mkubwa.
Naye Aaron Paul, aliyeigiza Jesse Pinkman, alieleza kuvunjika moyo kutokana na kumpoteza rafiki yake, huku Dean Norris akimkumbuka kama kijana mwenye moyo mzuri.

Breaking Bad ilikuwa miongoni mwa tamthilia zilizopata mafanikio makubwa duniani, ikipokea uteuzi 58 wa tuzo za Primetime Emmy na kushinda tuzo 16.
Kupitia uhusika wake na juhudi zake za kutetea ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, RJ Mitte aliacha alama katika tasnia ya burudani na katika mapambano ya kujenga jamii inayowapa watu wote nafasi sawa.
Discussion
Reader comments
0 contributions