Soka la Tanzania limeendelea kuandika historia katika mashindano ya kimataifa baada ya klabu nne, Simba SC, Young Africans (Yanga), Azam FC na Singida Black Stars kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa 2026/2027, mafanikio yanayoendelea kuonesha ukuaji wa soka la klabu nchini katika medani za kimataifa.
Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kurudia rekodi ya kuwa na timu nne katika hatua ya makundi ya mashindano makubwa ya klabu barani Afrika kwa msimu wa pili mfululizo, baada ya kufanya hivyo pia katika msimu wa 2025/2026.
Hatua hiyo imeongeza matumaini ya mashabiki wa soka nchini kuona klabu za Tanzania zikiendelea kufanya vizuri na kuimarisha nafasi ya nchi katika viwango vya mashindano ya klabu vinavyoratibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Droo ya hatua ya makundi iliyofanyika Jumatano, Oktoba 28, 2026 jijini Cairo, Misri, imeziweka klabu hizo katika makundi yenye ushindani mkubwa, huku Simba na Yanga zikiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Azam FC na Singida Black Stars zikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Young Africans imepangwa Kundi B pamoja na Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia.
Kundi hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa timu zenye historia na uzoefu wa mashindano ya Afrika, hususan Zamalek ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano.
Yanga inaingia katika hatua hiyo ikiwa na matumaini makubwa baada ya kuonesha uwezo mzuri kwenye michezo ya mchujo, ambapo iliiondoa CFFA ya Madagascar kwa jumla ya mabao 8-1. Hata hivyo, ili kufuzu robo fainali,
Wananchi watahitaji kutumia vizuri michezo yao ya nyumbani, kuimarisha safu ya ulinzi na kutafuta matokeo chanya wanapocheza ugenini dhidi ya wapinzani wao.

Kwa upande wa Simba SC, Wekundu wa Msimbazi wamepangwa Kundi C pamoja na RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Colombe Sportive ya Cameroon.
Simba imefuzu hatua hiyo baada ya kuiondoa 15 de Agosto ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 9-1, matokeo yanayoonesha uwezo wake wa kushambulia na kutumia nafasi za kufunga.
Hata hivyo, Simba inakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa RS Berkane na Orlando Pirates, ambazo zina uzoefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa.
Ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali, Simba itahitaji kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika michezo yake mitatu ya nyumbani na angalau kuvuna pointi muhimu katika baadhi ya michezo ya ugenini.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC imepangwa Kundi B pamoja na AS FAR ya Morocco, Al Ahly Tripoli ya Libya na Durban City ya Afrika Kusini.
Azam imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuiondoa ZED FC ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1, jambo linaloipa timu hiyo matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika hatua ya makundi.
Kwa Azam, changamoto kubwa itakuwa kuhakikisha inaonesha uimara dhidi ya AS FAR, huku michezo dhidi ya Al Ahly Tripoli na Durban City ikiwa na umuhimu mkubwa katika kuamua nafasi yake ya kufuzu hatua inayofuata.
Uwezo wa timu hiyo kucheza kwa nidhamu, kutumia nafasi za kufunga na kupata ushindi katika michezo ya nyumbani unaweza kuwa msingi wa mafanikio yake.
Wakati huohuo, Singida Black Stars imepangwa Kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Red Arrows ya Zambia.
Mpinzani wa nne atasubiri kuthibitishwa baada ya kukamilika kwa michezo ya kufuzu. Timu zinazohusishwa na nafasi hiyo ni CR Belouizdad ya Algeria, AS Douanes ya Mauritania na Hafia ya Guinea.
Singida Black Stars imefuzu hatua ya makundi kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuiondoa Tusker FC ya Kenya kwa jumla ya mabao 2-1.
Mafanikio hayo yanaipa klabu hiyo nafasi ya kuendelea kujenga heshima katika mashindano ya Afrika, lakini pia yanaongeza wajibu wa kuhakikisha inafanya vizuri zaidi na kuwania nafasi ya kufuzu robo fainali.
Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano ya CAF, kila kundi linajumuisha timu nne zinazocheza michezo sita kwa mfumo wa nyumbani na ugenini, huku timu mbili zitakazomaliza katika nafasi za kwanza na pili zikifuzu hatua ya robo fainali.
Hii ina maana kwamba Tanzania ina nafasi ya kinadharia ya kuingiza timu zote nne katika hatua ya robo fainali, ingawa kufikia mafanikio hayo kutategemea matokeo ya kila klabu katika kundi lake.
Licha ya rekodi ya kuingiza timu nne katika hatua ya makundi, mafanikio ya kweli kwa Tanzania yatapimwa kwa uwezo wa klabu hizo kufuzu hatua ya robo fainali na kuendelea kufanya vizuri katika hatua za mtoano.
Matokeo mazuri yanaweza pia kusaidia kuimarisha nafasi ya Tanzania katika viwango vya CAF, ambavyo hutumika kuamua idadi ya nafasi za uwakilishi wa nchi katika mashindano ya klabu barani Afrika.
Michezo ya hatua ya makundi inatarajiwa kuanza Novemba 27 hadi 29, 2026 na kukamilika Januari 2027, kabla ya hatua ya robo fainali kuanza Februari.
Kwa sasa, macho na matumaini ya mashabiki wa soka nchini yameelekezwa kwa Simba, Yanga, Azam FC na Singida Black Stars.
Swali kubwa ni kuwa, iwapo rekodi ya Tanzania kuingiza timu nne katika hatua ya makundi inaweza kugeuzwa kuwa historia mpya ya kuwa na timu nyingi zaidi zinazofuzu robo fainali ya mashindano ya CAF katika msimu mmoja.
Discussion
Reader comments
0 contributions