Baadhi ya viongozi wakiwa kwenye kiako cha kamati ya maafa Mkoa wa Kigoma .Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amezitaka Taasisi na mamlaka za Serikali Mkoani humo kuwa na mipango madhubuti na inayotekelezeka ya kukabiliana na maafa kabla hayajatokea huku akisisitiza usalama wa maisha ya wananchi kupewa kipaumbele.

Ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Dharura ya Maafa ya Mkoa wa Kigoma, kilichofanyika kwa lengo la kufanya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Amesema mipango yote iliyowekwa na kuazimiwa na mamlaka husika inapaswa kuanza kutekelezwa kwa vitendo, badala ya kubaki katika makabrasha bila utekelezaji.
“Tuanze utekelezji wa mipango na sio yabaki kwenye makablasha kwa sababu hii sio ya kuanza kusubiri ni jambo la dharura na hivyo liende kidharura sitegemei kusikia eti hakuna kinachofanyika wakati tumekubaliana” alisema Sirro.
Aidha, Balozi Sirro amewataka wananchi kushiriki katika kufanya usafi wa mifereji na mitaro ya maji ili kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi, hatua ambayo inaweza kusaidia kupunguza athari za mafuriko yanayoweza kusababishwa na kuziba kwa mifereji.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa, amezitaka Wilaya zote za Mkoa huo kuchukua tahadhari mapema na kutekeleza hatua za maandalizi bila kusubiri majanga yatokee na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinna Mathamani, amewataka wananchi kujiandaa kwa kuweka akiba ya chakula ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza endapo mvua hizo zitasababisha usumbufu wa shughuli za kila siku na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira kama sehemu ya hatua za kinga dhidi ya athari zinazoweza kutokana na mvua kubwa.
Discussion
Reader comments
0 contributions