Pato la Mkoa wa Singida limeongezeka kutoka Shilingi trilioni 3.5 mwaka 2023 hadi Shilingi trilioni 3.9 mwaka 2024, huku Mkoa ukiendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameyasema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkoa wa Singida katika Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Martha Moses Mlata.
Dendego amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 umejikita katika maeneo saba, ikiwemo uchumi, uzalishaji, afya, elimu na miundombinu, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema katika sekta ya kilimo, Mkoa umezalisha tani 1,005,544.3 za mazao ya chakula na tani 452,958.5 za mazao ya biashara, huku hekta 17,437 kati ya 48,619 zinazofaa kwa umwagiliaji zikiwa tayari zinatumika na hekta 10,980 zikiwa katika hatua mbalimbali za uendelezaji.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Mkoa wa Singida.
Dendego amesisitiza umuhimu wa kila mtendaji wa Serikali na Chama kuifahamu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuitumia katika utekelezaji wa majukumu, huku akiwapongeza wananchi wa Singida kwa kuendelea kutoa utulivu unaowezesha Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo.
Baadhi ya wanachma wa CCM Mkoa wa Singida wakifuatilia ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkoa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Moses Mlata, amempongeza Dendego kwa utekelezaji wa Ilani na kumtaka kuendelea kusimamia kwa nguvu utekelezaji wake ili wananchi wanufaike na maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata akizungumza kwenye ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkoa wa Singida.
Discussion
Reader comments
0 contributions