Katika kuhakikisha Mkoa wa Singida unajiandaa vyema kukabiliana na mvua za El Niño zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Ma-DAS wa Wilaya na Wakuu wa Taasisi za Serikali wamekutana kujadili mikakati ya maandalizi na utekelezaji wa majukumu katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Akufungua kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Rodrick Mpogolo, amesema Mkoa unapaswa kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na El Niño, huku kila taasisi na Halmashauri ikiwa na hatua za kuchukua kulingana na eneo lake. Amesema maandalizi yanapaswa kuhusisha pia miundombinu ya elimu wakati wa kuwapokea wanafunzi watakaomaliza darasa la sita mwaka 2027, pamoja na kuhakikisha huduma muhimu kwa wananchi zinaendelea kutolewa katika mazingira yoyote yatakayojitokeza.
Mpogolo amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Serikali unapaswa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo, sambamba na kutumia busara na hekima. Amesema Sekretarieti itafuatilia utekelezaji wa bajeti, ukusanyaji wa mapato ya ndani, matumizi na ufikaji wa fedha, hoja za ukaguzi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo, madeni ya watumishi na utoaji wa huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, maji, nishati na miundombinu. Pia amewataka waajiri kuhakikisha stahiki za watumishi zinalipwa ili kuongeza morali ya kufanya kazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Rodrick Mpogolo
Aidha, amesema wataalamu wanapaswa kuwa chanzo cha mawazo ya maendeleo ya Mkoa kwa kubuni fursa na mikakati ya kuimarisha ustawi wa wananchi na kuhakikisha wanaacha alama katika utekelezaji wa majukumu yao. Amewataka Halmashauri kujikita katika vyanzo vikuu vya uzalishaji kulingana na mazingira yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wa Singida wananufaika na fursa za uzalishaji, ikiwemo zao la alizeti ambalo lina mchango mkubwa katika kuongeza kipato, ajira na upatikanaji wa mafuta ya kula.
Aidha, kikao hicho kimejadili mkakati wa zao la alizeti, ambapo Bw. Mpogolo amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Singida.
Discussion
Reader comments
0 contributions