Na Saulo Stephen - Singida.
Mkoa wa Singida umeendelea kuimarisha utekelezaji wa utawala bora kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alipokuwa akiwakaribisha wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria waliofika mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Dendego amesema ujenzi wa jengo hilo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji haki.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Mkoa imeendelea kuweka mkazo katika kuimarisha utawala bora kwa kuongeza idadi ya watumishi wa umma katika sekta mbalimbali na kubuni mbinu mbadala za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aliongeza kuwa katika juhudi hizo, Mkoa unaendelea kunufaika na mchango wa wataalamu wanaojitolea huku halmashauri zote zikitenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wataalamu hao ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, alisema ziara ya kamati hiyo imelenga kukagua maendeleo ya mradi huo.

Lengo ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wake. Alisema kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo na inaamini mradi huo utakamilika kwa wakati kutokana na usimamizi mzuri pamoja na uongozi imara wa Mkoa wa Singida.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, alisema hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 32 ya utekelezaji na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.1 (2,102,417,178) hadi kukamilika kwake.
Discussion
Reader comments
0 contributions