Na Saulo Stephen - Singida.
Wananchi Manispaa Singida, wametakiwa kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia upatikanaji wa matibabu pindi wanapougua na kuepuka gharama kubwa za matibabu.
Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Jesca Lebba, wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Manispaa ya Singida kwa lengo la kujionea utoaji wa huduma za afya na kuzungumza na watumishi wa sekta hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Lebba amesema kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni suluhisho muhimu kwa wananchi kwani inawawezesha kupata huduma za matibabu wakati wowote wanapougua bila kubeba mzigo mkubwa wa gharama.
"Tunawahimiza wananchi wasisite kutoa taarifa wanapoona changamoto katika utoaji wa huduma za afya ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati na kuboresha huduma," amesema.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya mkoani Singida, akisema hatua hiyo imechangia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Dkt. Lebba ameahidi kuendelea kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye viwango vinavyostahili.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dkt Godfrey Andrew, amesema hospitali hiyo itaendelea kuboresha huduma za afya ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wakazi wa Manispaa ya Singida.
Discussion
Reader comments
0 contributions