Na Saulo Stephen – Singida.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Godfrey Mdama amesema Manispaa hiyo imeanza utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa kuboresha usafi wa mazingira kwa kubadili mfumo wa ukusanyaji taka katika maeneo mbalimbali ya mji wa Singida.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meya Mdama amesema mfumo huo mpya utahusisha matumizi ya vizimba vya taka, ugawaji wa maeneo maalum ya ukusanyaji pamoja na kupeleka magari ya taka moja kwa moja katika mitaa ili kuongeza ufanisi wa huduma hiyo.
Amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwepo kwa changamoto katika mfumo wa awali, ambapo baadhi ya vizimba vya taka vilikuwa vikibadilishiwa matumizi katika maeneo tofauti ikiwemo katika soko la Msufini, hali iliyokuwa ikikwamisha ukusanyaji wa taka kwa wakati.

“Mfumo huu mpya unalenga kuhakikisha taka zinakusanywa kwa ufanisi zaidi na mazingira ya mji wetu yanabaki kuwa safi muda wote,” amesema Meya Mdama.
Aidha amesema ongezeko la taka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa pamoja na mfumo wa awali kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, vimelazimu Manispaa kuanzisha utaratibu huo mpya wa ukusanyaji taka.
Katika hatua nyingine, Manispaa ya Singida imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutunza mazingira kwa kutumia maeneo rasmi ya kutupia taka, hatua itakayosaidia kuhakikisha mji wa Singida unakuwa safi na salama kiafya.
Discussion
Reader comments
0 contributions