Na Saulo Stephen - Singida.
Ujenzi wa Barabara ya Noranga (Doroto)–Itigi (Mlongojii) yenye urefu wa kilomita 25 katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida umefikia asilimia 83.25, hatua inayotarajiwa kuimarisha usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao katika ukanda wa kati wa Tanzania.
Taarifa hiyo imetolewa mbele ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, alipokagua maendeleo ya mradi huo Mei 31, 2026. Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko, alisema kilomita 20.2 tayari zimekamilika kwa kiwango cha lami huku kilomita 4.8 zilizobaki zikitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2026.

Kwa mujibu wa TANROADS, barabara hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa Barabara ya Mbeya–Chunya–Makongolosi–Rungwa–Itigi–Mkiwa yenye kilomita 524 inayounganisha mikoa ya Mbeya, Singida na Tabora. Kukamilika kwake kunatarajiwa kufungua fursa zaidi za biashara na kurahisisha huduma za usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 29.6 unatekelezwa na China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa ufadhili wa asilimia 100 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi za ujenzi zilianza Septemba 2022 na zinatarajiwa kukamilika Agosti 7, 2026.

Mbali na kuboresha miundombinu, mradi huo umechangia ajira kwa wananchi ambapo watu 305 wameajiriwa, kati yao 278 ni wazawa sawa na asilimia 91 ya ajira zote zilizotolewa.
Aidha, wananchi 578 walioathiriwa na utekelezaji wa mradi huo wamelipwa fidia ya jumla ya shilingi milioni 721.4, hatua iliyowezesha kuendelea kwa ujenzi kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.

Kukamilika kwa barabara hiyo kunatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo ya Itigi, Manyoni na mikoa inayounganishwa na mradi huo.
Discussion
Reader comments
0 contributions